Polisi yaua watatu kwa risasi Serengeti

What you need to know:

  •  Watu watatu wameuawa na polisi wakidaiwa kuwa ni majambazi.


Musoma. Watu watatu wameuawa na polisi wakidaiwa kuwa ni majambazi.

Akizungumzia tukio hilo jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tibishiwanu alisema watu hao wameuawa kwa kupigwa risasi baada ya kujaribu kuwatoroka askari usiku wa kuamkia jana.

Alidai kuwa walikamatwa kwenye operesheni iliyofanywa kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara, Mwanza, Simiyu na Kanda maalumu ya Tarime/Rorya kufuatia matukio ya ujambazi wa kutumia silaha, matukio yanayodaiwa kufanywa na watuhumiwa hao wakishirikiana na wenzao.

‘‘Hawa watu wameanza kutusumbua tangu mwezi wa sita, katika matukio hayo walikuwa wakijeruhi na kuiba ndipo tukaamua kufanya operesheni ya pamoja kuwasaka,” alidai kamanda huyo.

Alisema juzi waliwakamata watu wanne ambao baada ya kufikishwa kituo cha polisi walikiri kuhusika na matukio ya ujambazi na wakawataja wenzao watatu waliokuwa wakishirikiana nao.

“Usiku watuhumiwa hao waliwaongoza polisi kwenda kuwaonyesha walipojificha wenzao watatu, lakini walipofika Kitongoji cha Gentamome majira ya saa 8 usiku, ghafla askari hao walishambuliwa na risasi kutoka maporini, nao wakajibu mapigo,” alisema Kamanda Tibishiwanu.


Walichosema wananchi

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu jana, Katibu wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), Catherine Ruge alisema kuwa miongoni mwa waliouawa yumo mjomba wake.

Ruge alidai kuwa magari mawili ya Polisi yalifika nyumbani kwa mjomba wake huyo katika kijiji cha Majimoto wilayani Serengeti asubuhi ya Septemba 21 na kumkamata mjomba wake huyo aitwaye Mgale Mikori, wakidai kuwa kuna operesheni ya kusaka majambazi katika wilaya hiyo.

“Walisema wanampeleka Mugumu mjini na kwa vile kule ni mbali zaidi ya kilomita 80, ndugu zangu hawakuweza kwenda jana hiyo hiyo kituoni, ikabidi leo ndipo wakatumwa watu kumpelekea chai pale kituoni Mugumu,” alisema.

Alisema kuwa baada ya ndugu hao kufika na kumuulizia huyo mjomba wake, polisi waliokuwepo kituoni hapo walisema, mtu huyo hayupo kituoni hapo jambo ambalo liliwashangaza na hivyo kuanza kuwasiliana na ndugu wengine ili kujua ndugu yao alipo.

“Walimpigia kaka yake marehemu ambaye pia alimpigia simu askari mmoja na alipomueleza shida yake yule askari alimuuliza unawatafuta wale majamabazi kama ni hao hebu nendeni mochuari mkaangalie,” alisema

Baada ya taarifa hizo ndugu hao walikwenda katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Wilaya ya Serengeti ambapo walikuta miili ya watu wanne ikiwa imelazwa sakafuni bila nguo ukiwamo mwili wa mjomba wake huyo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamwehuru wilayani Serengeti,David Mgendi, alidai kuwa asubuhi ya usiku wa kuamkia Septemba 22, alipoamka alipigiwa simu na wananchi wakimueleza kuhusu milio ya risasi iliyosikika kijijini hapo.

“Nilipoamka asubuhi nilipigiwa simu na wananchi wangu wakanieleza kuhusu milio ya risasi iliyosikika usiku wa kuamkia leo (jana) ikabidi niende eneo la tukio na kweli nilikuta damu nyingi sana hata ukienda sasa hivi utakuta damu zimeganda pale,” alisema.

Mwenyekuti huyo alifafanua kuwa kwa mujibu wa wananchi hao, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Septemba 22 saa 9 alfajiri na lilidumu kwa takriban dakika tano na kwamba muda wote wa tukio hakuna mwananchi aliyeweza kutoka nje.

Alisema kuwa milio mingi ya risasi ilisikika na kufafanua kuwa kabla ya kuanza kusikika milio hiyo zilisikika sauti za watu zikizuia watu wengine kutokukimbia na kutoroka.

“Walisikika wakisema mnaenda wapi rudini hapa mnataka kukimbia na baada ya muda milio ya risasi ikaanza kusikika kwa fujo jambo ambalo lilizua hofu kwa wakazi wa maeneo yalipotokea tukio hilo na kuendelea kujifungia ndani kwa sababu hawakujua nini kinaendelea” alisema.

Alidai kuwa tukio hilo limetokea jirani na lambo la maji lililopo kijijini hapo hatua 10 kutoka barabara ya kwenda katika kijiji cha jirani cha Marasomoche na kwamba hadi sasa hawajui ni nini kilichotokea usiku huo.


Uongozi wa wilaya

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dk Vicent Mashinji alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema kuwa yupo likizo na kumtaka mwandishi wa habari kuwasiliana na kamanda wa polisi mkoa wa Mara kwa ajili ya ufafanuzi.