Pori la Selous larudishwa urithi wa dunia

Tuesday July 20 2021
pori pc

Katibu Mkuu Wizara ya maliasili na Utalii,Dk Allan Kijazi

By Amina Ngahewa

Arusha. Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Allan Kijazi amesema Serikali kwa kushirikiana na wataalamu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) waliopo hapa nchini wamefanikiwa kuirudisha Pori la Akiba la Selous ili iendelee kuwepo kwenye orodha ya maeneo ya urithi wa dunia.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kikao kazi kilichoendeshwa kwa njia ya mtandao na kuhudhuriwa na nchi wanachama  21  Dk Kijazi amesema taarifa zilizokuwa zimetumika kutaka Selous iondolewa kwenye orodha zilikuwa sio sahihi kwa kuwa zilikuwa zimetegemea  kusikia na sio kupata taarifa kamili kutoka kwa nchi husika.

"Kama ambavyo tuliripoti wakati  wa mkutano wa Unesco ulipoanza kulikuwa na mapendekezo ya Selous kuondolewa kwenye  orodha ya maeneo ya urithi wa dunia  sisi na wataalamu tumekaa na kuona taarifa zilizotumika si sahihi na zilikuwa na uongo mwingi," amesema.

Dk Kijazi aliongeza kuwa mapendekezo ambayo yalikuwa yametolewa na IUCN pamoja na World Heritage Central ambayo yalitumika  kuishauri Unesco kuiondoa Selous yalikuwa hayajafuata utaratibu kwa kuwa walikuwa hawajashirikishwa  kitu ambacho ni tofauti na miongozo walikubaliana kwenye kuchagua na kusimamia maeneo hayo .

"Wataalamu wamefanya kazi kubwa kueleza ukweli kuhusu hali ilivyo na kuziambia nchi wanachama ishirini na moja ambazo zinapiga kura kuwa utaratibu umekosea na taarifa zilizotolewa sio sahihi  kwa hiyo Selous iendelee kubaki na kuwaomba IUCN pamoja na World Heritage Central kukusanya taarifa zenye usahihi na sio za kupotosha dunia" aliongeza

Kwaupande wake Profesa Hamisi Malebo ambaye ni  Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Unesco  kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema taarifa iliyokuwa imetolewa ilikuwa imetiwa chumvi kwa kuwa walikuwa wamesema Selous ilikuwa imepoteza sifa kwa kuwa wamefyeka miti yote na kusababisha uharibifu kitu ambacho sio kweli kwakuwa eneo lililokuwa limefyekwa ni dogo sana .

Advertisement
Advertisement