Prince Harry, Meghan kuanza Netflix na Invictus Games

Thursday April 08 2021
MEGANIPIC

Los Angeles, Marekani (AFP). Prince Harry atatayarisha makala kuhusu michezo ya wanajeshi maveterani waliolemaa (Invictus Games), ikiwa ni mfululizo wa kwanza wa filamu chini ya mkataba mnono ambao yeye na mkewe Meghan Markle wamesaini na kampuni ya mtandaoni ya Netflix baada ya kuhamia California mwaka jana.

Mjukuu huyo wa malkia wa Uingereza, ambaye alilitumikia jeshi la nchi hiyo nchini Afghanistan, ataonekana katika kamera na pia kuwa mtayarishaji mtendaji wa mfululizo wa filamu hiyo ya "Heart of Invictus," ambayo ina sehemu nyingi zinazofuata wanamichezo walemavu wanajeshi wakati huu wakijiandaa kwa michezo yao itakayofanyika The Hague.

"Filamu hii itaipa jumuiya kote duniani nafasi ya kujua habari za kuwanyanyua na za kusisimua za washindani hawa wakati wakielekea Uholanzi mwakani," alisema Harry katika taarifa yake.

Programu hiyo itakuwa ya kwanza kutolewa na kampuni ya wanandoa hao ya Archewell Productions, ambayo ilisaini mkataba huo mnono Septemba mwaka jana na Netflix ambayo huonyesha filamu zake kwa njia ya mtandao.

"Kama mfululizo wa kwanza kwa Archewell Productions pamoja  na Netflix, na kwa ushirikiano na Taaisisi ya Invictus Games, ninafurahia zaidi safari iliyo mbele na najivunia jumuiya ya Invictus kwa kuendelea kuongoza kuitibu dunia," alisema Prince Harry.

Hakuna taarifa zozote za kifedha zilizotolewa, lakini mkataba huo umeripotiwa kuwa wa miaka mingi na wenye haki peke kwa Netflix.

Advertisement
Advertisement