Prof. Lipumba: Maalim Seif alinifundisha siasa za Zanzibar zinazoelezeka, zisizoelezeka

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Nilipokea kwa masikitiko, simanzi na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Maalim Seif Shariff Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo.

Nilipokea kwa masikitiko, simanzi na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Maalim Seif Shariff Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo.

Mara ya kwanza nilikutana na Maalim Seif kati ya Julai na Agosti 1973, msikitini tukiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kipindi hicho nilikuwa mwaka wa kwanza Idara ya Uchumi, Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii.

Maalim Seif yeye alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili, Idara ya Sayansi ya Siasa, Utawala na Uhusiano wa Kimataifa.

Wakati huo idadi ya wanafunzi wa Kiislamu tuliokuwa tunasali kila siku idadi yetu ilikuwa ndogo sana. Tulikuwa hatujazi safu hata moja.

Na kila nikienda kusali, nilimkuta Maalim Seif. Baada ya sala aliendelea na dua na kuvuta nyiradi. Tulizoeana kwa kukutana mara nyingi msikitini na tulikuwa tukizungumza kwa muda mrefu baada ya sala ya usiku.

Nilijifunza historia ya siasa za Zanzibar - zinazoelezeka na zisizoelezeka toka kwake.

Mwaka 1974 tulimchagua Maalim Seif kuwa mwenyekiti wa umoja wa wanafunzi wa Kiislamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (MSAUD).

Sitna Mohamed kwa sasa ni marehemu, alichaguliwa kuwa katibu na mimi nilichaguliwa kuwa mtunza hazina, japo hatukuwa na hazina ya kutunza.

Shughuli yetu kubwa ilikuwa kuhakikisha Mwezi wa Ramadhani tuna futari nzuri na daku pia.

Aidha, tuliwakaribisha wahadhiri wa Kiislamu kutoka maeneo mbalimbali kutoa mihadhara.

Maalim Seif alimaliza kidato cha sita mwaka 1963, baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, hakupewa fursa ya kuendelea na masomo ya chuo kikuu.

Badala yake alipangiwa kazi ya ualimu na kwa miaka kadhaa, alikuwa mwalimu wa shule za sekondari. Hicho ndicho chanzo cha yeye kufahamika kwa jina la Maalim.

Tanzania Bara tunatumia msamiati wa ‘Maalim’ kwa walimu wa madrasa na viongozi wa dini ya Kiislamu. Tofauti na Bara, Zanzibar walimu wa skuli au shule za kisekula ndiyo wanaitwa ‘Maalim’.

Wanafunzi kutoka Zanzibar walianza kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1972. Maalim alikuwa miongoni mwa wanafunzi hao na alikuwa kiongozi wao.

Baadhi ya wanafunzi hawa ni pamoja na Juma Duni Haji, Omari Ramadhani Mapuri, Marehemu Abubakar Khamis Bakari na wengine.

Karibu wanafunzi wote alioingia nao Chuo Kikuu mwaka 1972, alikuwa amewafundisha Skuli za Sekondari Zanzibar.

Mwaka 1975 nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TANU Youth League, Wilaya ya Mlimani.

Wakati wanafunzi Wazanzibari wakisherehekea sikukuu ya Mapinduzi pale chuoni kwenye ukumbi wa Baraza la Chuo, Maalim alinialika kushiriki na kutoa salamu za vijana wa TANU.

Na alipofika mwaka wa tatu karibu na kufanya mitihani ya mwisho, Maalim aliugua na kulazwa zahanati ya Chuo Kikuu.

Kila jioni nilikwenda kumjulia hali. Mitihani ya mwisho ya mwaka wa tatu ilibidi aifanyie kwenye chumba alikolazwa.

Pamoja na kuwa alikuwa mgonjwa, lakini alifaulu vizuri na kuongoza katika Idara ya Sayansi ya Siasa.

Katika mazingira hayo magumu, Maalim Seif alipata shahada yake ya B.A daraja la juu (B.A. Hon First Class).

Walimu wake wa Chuo Kikuu na hasa Profesa Goran Hyden (raia wa Sweden) na Marehemu Nathan Shamuyarila (Mzimbabwe aliyekuja kuwa Waziri wa Mambo ya Nje baada ya Uhuru wa Zimbabwe 1980), walijaribu kumshawishi Maalim abakie Chuo Kikuu kama Mkufunzi Msaidizi na hatimaye kuendelea na masomo ya juu, lakini alichagua kuitikia wito wa kurudi Zanzibar na kwenda kuwa Msaidizi wa Rais wa Zanzibar enzi hizo, Aboud Jumbe.

Mimi nilimaliza shahada ya kwanza 1976 na nikaajiriwa kama Mkufunzi Msaidizi, Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Baadaye kidogo nilipata fursa ya kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Stanford, nchini Marekani.

Niliporejea nchini 1983, hali ya uchumi ilikuwa ngumu. Kila bidhaa ilikuwa adimu isipokuwa majani ya chai.

Kuanzia 1984, Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu ilikuwa inafanya makongamano ya sera za uchumi za kupambana na hali ngumu ya maisha.

Akiwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, Maalim Seif alisimamia sera ya kulegeza masharti ya kufanya biashara na kuimarisha upatikanaji wa bidhaa Zanzibar.

Sera za kurekebisha uchumi, hasa katika biashara, zilianza kutekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kabla ya Serikali ya Muungano, kwa sababu ya ushawishi wa Maalim Seif Sharif Hamad.

Miaka ya 1970 na 1980, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilikuwa na utamaduni wa kufanya mkutano kila mwaka kuhusu harakati za Ukombozi Kusini mwa Afrika.

Maalim Seif afariki dunia

Toka akiwa Chuo Kikuu, Maalim Seif alikuwa mtafiti na mfuatiliaji wa ukombozi wa Bara la Afrika. Mwaka 1986 akiwa Waziri Kiongozi, alikuwa Mgeni Rasmi kwenye ufunguzi wa mkutano wa Ukombozi wa Kusini mwa Afrika jijini Arusha.

Wakati huo, Makaburu walikuwa wanatawala na kuendeleza siasa za ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini na Namibia. Nakumbuka Maalim alitoa hotuba iliyosisitiza kuwa nchi za Kiafrika hazitakuwa huru mpaka makaburu wang’olewe Namibia na Afrika ya Kusini.

Alisema huo ni wajibu wa nchi zote za Afrika kuunga mkono juhudi za ukombozi.

Maalim Seif aliondolewa kwenye nafasi ya Waziri Kiongozi na kufukuzwa uanachama wa CCM na akawekwa ndani mwaka 1988.

Nikiwa Chuo Kikuu mwaka 1989 niliishawishi Jumuiya ya Walimu (UDASA) kutoa Tamko la kuitaka serikali kumuachia huru Maalim Seif.

Nakumbuka aliyeandika rasimu ya mwanzo ya tamko hilo, alikuwa Profesa Hamza Njozi, wakati huo akiwa Mhadhiri Idara ya Kiingereza, na baadaye akaja kuwa Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislam, Morogoro.

Sikupata fursa ya kukutana na Maalim Seif mwanzoni mwa miaka ya 1990. Mwaka 1991 niliteuliwa rasmi kuwa Mshauri wa Rais Mwinyi kuhusu masuala ya Uchumi.

Mwaka 1993 nikapewa fursa ya kuwa Fulbright Visiting Professor of Economics, Williams College, Massachussets, Marekani. Niliporudi toka Marekani Julai, 1995 wakati tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu ndipo uhusiano wa kisiasa na Maalim Seif ulipoanza rasmi.

Nje ya siasa Maalim Seif alikuwa nani?

Imeandikwa na Profesa Ibrahim Lipumba