Prof Mwaikambo atoa wito kwa wahitimu wa taaluma ya afya nchini
Wahitimu wa shahada ya maabara katika chuo kikuu kishiriki cha Kikristo cha Tiba, Kilimanjaro(KCMUCo) wakila kiapo. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Wahitimu wa kada mbalimbali za afya hapa nchini wametakiwa kutumia taaluma zao kutoa huduma zisizo na dosari na zinazoweza kusababisha madhara kwa binadamu na kufuata maadili msingi ya utumishi wa sekta ya afya bila ubaguzi na kuzingatia neno la Mungu.
Moshi. Wahitimu wa kada mbalimbali za afya hapa nchini wametakiwa kutumia taaluma zao kutoa huduma za afya zisizo na dosari na zinazoweza kusababisha madhara kwa binadamu na kufuata maadili msingi ya utumishi wa sekta ya afya bila ubaguzi na kuzingatia neno la Mungu.
Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa baraza la chuo kikuu cha Tumaini Makumira, Profesa Esther Mwaikambo wakati wa mahafali ya 23 ya Chuo Kikuu Kishiriki cha kikristo cha tiba, Kilimanjaro (KCMUCo) ambapo jumla ya wahitimu 176 wamehitimu fani mbalimbali za afya.
Profesa Mwaikambo amewataka wahitimu hao kuonyesha umahiri katika kutoa huduma kwa jamii na kuonyesha upendo kwa wagonjwa na kwamba kwa kufanya hivyo watakuwa mabalozi wazuri wa chuo hicho.
"Nitoe wito kwa wahitimu wote, muonyeshe umahiri katika kutoa huduma zenu za afya na siku zote mkumbuke dhamira yetu ya kutosababisha madhara kwa biandamu yoyote,"Amesema Profesa Mwaikambo
"Mkumbuke siku zote kutenda kazi zenu kwa kufuata maadili msingi ya watumishi wa sekta yetu ya afya bila ubaguzi kwa kuzingatia neno la Mungu maana wagonjwa wanahitaji huruma na uvumilivu mkubwa kutoka kwenu naomba msituangushe,"
Pamoja na mambo mengine amesema, chuo hicho kwa sasa kimeanza kufanya udahili wa kozi 21 zilizofungiwa na Tume ya Vyuo Vikuu Nchini(TCU) na kwamba jitihada za kusomesha wataalam katika chuo hicho zinaendelea.
"Chuo kimeanza udahili wa kozi 21 zilizokuwa zimefungiwa na TCU na hadi sasa ni kozi nne tuu ambazo hazijaruhusiwa kuanza kudahili wanafunzi kutokana na kukosekana kwa wataalam wa kutosha wenye sifa hizo hapa nchini na nchi jirani,"
"Mwaka huu wa masomo chuo kinasomesha madaktari zaidi ya 45 wa fani za uzamivu, uzamili hapa nchini na nje ya nchi kwa lengo la kuongeza uwezo wa kitaaluma katika fani mbalimbali,"
Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Ephata Kaaya, amewataka wahitimu hao wa kada za afya wanatumia viapo vya taaluma zao kwa kuzingatia maadili ya huduma watakazozitoa kwa wagonjwa.
"Mafanikio yenu mema kwenye jamii yanatokana na Mungu kwa kuonyesha upendo kwa wagonjwa popote mtakapotoa huduma za afya, muwe mabalozi wazuri kwa kutoa huduma zisizo na dosari, mkitimiza haya Mungu atawabariki,"amesema Profesa Kaaya
Naye, Makamu Mkuu wa chuo kikuu cha Tumaini Makumira, profesa Joseph Parsalaw amewataka wahitimu hao kutumia vizuri taaluma zao kwa upevu wa akili katika kuhudumia jamii kwa kuwa inawategemea na kuwaamini sana..
"Mtumie vizuri taaluma zenu na upevu wa akili katika kuhudumia jamii, jamii inawaamini sana na inawategemea , malipo mtakayopata ni shukrani tu, fanyeni kazi kwa bidii na kwa uadilifu na kwa kufanya hivyo mtatukuka katika utumishi wenu,"
Claurence Mbore mmoja wa wahitimu wa shahada ya maabara, akaiomba serikali iangalie namna ya kutoa ajira kwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakihitimu katika fani mbalimbali lakini tatizo linakuwa ni ajira.
"Tunaomba Rais Samia Suluhu Hassan aweze kutoa nafasi za ajira kwa sisi wahitimu maana ni wengi wako mtaani hawana ajira, hapa tunamaliza chuo tunaenda mtaani lakini mwisho wa siku tunaomba ajira zitoke ili tuweze kuajiriwa,"