Profesa Lipumba: Hali ya uchumi Tanzania hairidhishi

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba amezungumza na wanachama wa CUF visiwani Zanzibar amegusia mambo mbalimbali ikiwamo hali ya uchumi wa Tanzania

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba amesema hali ya uchumi Tanzania hairidhishi na kwamba wananchi wanaishi kwenye maisha yasiyokua bora kinyume na matarajio.

Profesa Lipumba ambaye pia ni mbobezi wa uchumi ameyasema hayo leo Jumamosi Aprili 13, 2019 Unguja visiwani Zanzibar wakati akizungumza na viongozi pamoja na wanachama wa chama hicho katika mkutano maalumu uliofanyika Amani mjini hapa.

Amesemea hivi sasa maeneo mengi ya Tanzania hakuna mzunguko mzuri wa fedha hali ambayo imesababisha Watanzania walio wengi mijini na vijijini kuishi kwenye mazingira ya umaskini.

Hata hivyo, Profesa Lipumba amesema uwepo wa hali hiyo haukuwagusa wananchi wa kawaida pekee bali hata wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo na ndio maana biashara nyingi hivi sasa hazifanyi vizuri.

“Wafanyabiashara wadogo wakubwa wote wako hoi taabani hivi sasa jambo ambalo linasikitisha kwa nchi yenye rasilimali nyingi kama Tanzania,” amesema Lipumba.

Kutokana na mazingira hayo ameleza dhamira ya chama chao ikiwa ni kuitumia fursa hiyo na kuwaeleza wananchi sababu ya wao kuchaguliwa na kushika madaraka hatimaye waweze kuondoa changamoto hiyo.

Profesa Lipumba amesema kwa changamoto hiyo ambayo imeikabili Tanzania chama chao kitahitaji kuweka wagombea bora na wenye uwezo watakaoweza kunadi sera zenye kuleta tija kwa wananchi wote.