Profesa Luoga abashiri ukuaji wa uchumi Kanda ya Ziwa

Muktasari:

  • Gavana wa BoT amesema pato la Taifa litaongezeka kukana na uwekezaji unaoendelea wa viwanda katika Kanda ya Ziwa nan chi za jirani.

Mwanza. Mchango wa Pato la Taifa Kanda ya Ziwa unatarajiwa kuongezeka kutokana na uwekezaji unaoendelea katika ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya madini na ongezeko la biashara na nchi jirani.

 Akitoa salamu wakati wa ufunguzi wa jengo la ofisi za Benki Kuu (BOT) tawi la Mwanza leo Juni 13, 2021 Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Florens Luoga amesema ongezeko la biashara ni kwenye mifugo, vyakula vya mifugo na bidhaa za viwandani na kilimo.

Amesema, pato la Mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa mwaka 2019 ni Sh34 bilioni sawa na asilimia 25.9 ya pato la taifa

Licha ya pato la mikoa ya Kanda ya Ziwa kuwa asilimia 25.9, Luoga amesema kanda ya ziwa pia uzalisha zaidi ya asilimia 90 ya dhahabu yote nchini, asilimia 50 ya pamba na Kahawa na zaidi ya asilimia 95 ya mauzo ya samaki ndani na nje ya nchi.

“Kumalizia ujenzi wa reli ya kisasa utachangia zaidi ukuaji wa kiuchumi katika kanda hii ya ziwa na nchi kwa ujumla,”

Amesema, BOT ina matawi manne ya Mwanza, Mtwara, Mbeya na Arusha huku tawi la Mwanza likihudumia mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara,Simiyu, Geita, Kagera na Kigoma.

Jengo hilo lenye ghorofa tano limegharimu zaidi ya Sh42.1 bilioni , Sh23.7 bilioni zikitumika kujenga jengo hilo na Sh18.73 bilioni zikitumika kufunga mitambo kwenye jengo hilo.