Profesa Mbarawa atoa maagizo kwa wahandisi

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Tanzania, Profesa Makame Mbarawa akizungumza katika siku ya wahandisi.

Muktasari:

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Tanzania, Profesa Makame Mbarawa amewataka wahandisi kufanya kazi zao kwa kuzingatia weledi na kujiepusha na udanganyifu.

Dodoma. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Tanzania, Profesa Makame Mbarawa amewataka wahandisi kufanya kazi zao kwa kuzingatia weledi na kujiepusha na udanganyifu.

 Profesa Mbarawa ameyasema hayo leo Alhamis, Septemba 22, 2022 wakati wa siku ya wahandisi nchini humo.

Amesema wahandisi kujipushe na vitendo vyote vya rushwa na udanganyifu, na ndiyo sababu katika taaluma yenu hii mnakula kiapo.

“Mnapewa dhamana ya kusimamia miradi mikubwa inayotumia fedha nyingi. Jitahidini kukamilisha miradi yote kwa uadilifu na kwa muda uliopangwa na kwa thamani iliyo halisi,”amesema.

Aidha, Profesa Mbarawa ameiagiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kuwachukulia hatua hatua stahiki na za haraka kwa makampuni ya kihandisi, taasisi na wahandisi wasio waadilifu ikiwa ni pamoja na kuwafutia usajili wao.

Msajili wa ERB, Benard Kavishe amesema wahandisi 36 wakiwemo 10 wa kike walizofanya vizuri watazawadiwa katika siku hiyo.

Amesema kuna uwiano usioridhisha wa usawa wa kijinsia kwa wahandisi na hivyo bodi inafanya jitihada kuhakikisha inakabiliana na tatizo hilo.

Amesema miongoni ni kutoa upendeleo wa utoaji wa mikopo kwa wahandisi wa kike na hosteli kuanzia shuleni hususani kuanzia kidato cha pili.

Pia, amesema bodi inapitia mpango wa mabadiliko ya Sheria utakayotaka miradi ijumuishe na fedha za mafunzo.