Profesa Mkenda aagiza kiwanda kuzalisha mbolea usiku na mchana

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda (kushoto) akizungumza na Mkurugenzi wa kiwanda cha mbolea cha Minjingu, Tosky Hans kilichopo wilayani Babati mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda ameutaka uongozi wa kiwanda cha mbolea cha Minjingu kuzalisha mbolea yao mchana na usiku ili kukidhi mahitaji ya bidhaa hiyo

Babati. Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda ameutaka uongozi wa kiwanda cha mbolea cha Minjingu cha wilayani Babati mkoani Manyara kufanya kazi mchana na usiku ili kuzalisha kiasi kikubwa cha mbolea.

Profesa Mkenda ameyasema hayo leo Oktoba 8, 2021 alipotembelea na kukagua shughuli za uzalishaji wa kiwanda hicho kilichopo kwenye Kata ya Nkaiti.

Amesema endapo kiwanda hicho kikifanya kazi mchana na usiku, uzalishaji wa mbolea utakuwa mkubwa hivyo kuwanufaisha wakulima nchini kutokana na mahitaji yake.

"Mahitaji ya mbolea ni makubwa nchini hivyo tekelezeni hilo kwani hata soko la walaji ni kubwa kutokana na wakulima wetu nchini kuitumia," ameagiza Profesa Mkenda.

Amesema mbolea hizo zinaweza kuhifadhiwa kwenye maghala ya Serikali wakati wa usambazaji na kiwanda hicho kikachangia gharama kwa kulipia kiasi cha fedha.


Hata hivyo, ameupongeza uongozi wa kiwanda cha Minjingu, kwa kuzalisha mbolea mpya ya zao la tumbaku, ambayo itawanufaisha wakulima wa zao hilo.

"Tutakuwa tunatoa mbolea ya tumbaku hapa Minjingu, tutaongeza ajira kwani tunapoteza fedha nyingi za kigeni kwa kuagiza mbolea ya tumbaku nje ya nchi," amesema Profesa Mkenda.

Mkurugenzi wa kiwanda cha mbolea cha Minjingu, Tosky Hans amesema watatekeleza agizo hilo la Serikali na kuuza mfuko mmoja wa mbolea wa kilo 50 kwa Sh55, 000.

Hans amesema hata mbolea ya Minjingu ikisafirishwa kwenda maeneo mbalimbali nchini hawatawazidisha bei ya Sh65, 000.