Profesa Mkenda amsimamisha kazi Mrajisi

New Content Item (3)
Profesa Mkenda amsimamisha kazi Mrajisi

Muktasari:

Kushindwa kutatua changamoto kwenye chama cha msingi, kumemweka matatani Mrajisi Msaidizi wa mkoani Lindi.

Dodoma. Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda amemsimamisha kazi Mrajisi Msaidizi wa Chama cha Ushirika mkoa wa Lindi, Edmund Massawe kwa kushindwa kutatua changamoto ndani ya chama hicho.

Pia, Profesa Mkenda amemweka chini ya uangalizi Mrajisi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kwa kushindwa kuwasilisha taarifa kuhusu namna ya kushughulikia changamoto ya Chama cha Ushirika Kilimanjaro (KNCU).

Akizungumza leo Alhamis ya Mei 13 2021, Profesa Mkenda amesema Massawe alishindwa kutatua changamoto ya Amcos iliyopo wilayani Liwale iliyohusu kulazimishwa kutumia ghala la kuhifadhia mazao la mtu binafsi.

Amesema Amcos hiyo ilikatazwa kutumia ghala lake na kutakiwa kutumia ghala la mtu binafsi kuhifadhia mazao.

Hata hivyo, amesema mbunge wa jimbo hilo alimtafuta na kumweleza kuhusu jambo hilo na alipomtafuta Masawe alisema atalishughulikia.

Amesema kutokana na changamoto hizo ambazo zilimlazimu kuingilia kati kuzitatua, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, kupeleka mrajisi mwingine mkoani Lindi.

“Uwezo wa kumngoa ninao, watch out (angalie)....ahakikishe hiyo taarifa inanifikia Jumatatu,”amesema Profesa Mkenda.