Profesa Mkenda: Halmashauri 17 zina upungufu wa chakula

Sunday October 17 2021
Mkenda pc

Waziri wa kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na baadhi ya wazalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula yanayozalishwa hapa nchni wakati alipokuwa akikagua mabanda ya maonyesho wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya chakula duniani yaliyofanyika leo mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph

By Janeth Joseph
By Fina Lyimo

Moshi. Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda amesema pamoja na nchi kuwa na utoshelevu wa chakula bado kuna halamshauri 17 kwenye mikoa 8 yenye upungufu wa chakula nchini.

Profesa Mkenda ameyasema hayo leo Oktoba 17, 2021 wakati akifunga kilele cha maadhimisho ya siku ya chakula duniani yaliyofanyika Kitaifa mkoani Kilimanjaro katika viwanja vya Mandela vilivyopo Manispaa ya Moshi.

Amesema hali hiyo inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo mtawanyiko mbaya wa mvua na visumbufu vya mazao shambani vilivyojitokeza wakati wa uzalishaji mwaka huu.

"Serikali inaendelea kufuatilia kwa ukaribu hali ya usalama wa chakula katika maeneo haya ili kuhakikisha utengamano wa hali ya chakula nchini unaendelea kuimarika,"amesema Profesa Mkenda.

Profesa Mkenda amesema ili kuhakikisha utengamano wa hali ya chakula nchini unaendelea kuimarika Wizara inaendelea kuratibu upatikanaji wa pembejeo kwa msimu ujao wa mwaka 2021/22 kwa wakati ikiwemo mbegu bora, mbolea na viatilifu.


"Serikali imechukua hatua kadhaa za lazima za kuimarisha sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya utafiti wa mbegu na kilimo bora kutoka sh.7.35 bilioni mwaka 2020/21 hadi sh.11.63 mwaka 2021/22"amesema Profesa Mkenda.

Advertisement


Ameongeza "Tumeongeza bajeti ya uzalishaji wa mbegu bora za kutosha na kwa bei nafuu hivyo Serikali kupitia wakala wa mbegu nchini imeongeza bajeti kutoka sh.5.42 bilioni hadi sh.10.58 bilioni kwa mwaka wa fedha 2021/22,"amesema Profesa Mkenda.

Advertisement