Profesa Sedoyeka: Kuna mafanikio udhibiti moto mlima Kilimanjaro
Muktasari:
- Wakati vikosi mbalimbali vya majeshi nchini vikiongeza nguvu kuzima moto katika mlima Kilimanjaro, Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Profesa Eliamani Sedoyeka amesema hadi kufika leo Jumapili Oktoba 23, 2020 jioni kutakuwa na mafanikio makubwa ya kudhibiti moto huo.
Moshi. Wakati vikosi mbalimbali vya majeshi nchini vikiongeza nguvu kuzima moto katika mlima Kilimanjaro, Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Profesa Eliamani Sedoyeka amesema hadi kufika leo Jumapili Oktoba 23, 2020 jioni kutakuwa na mafanikio makubwa ya kudhibiti moto huo.
Miongoni mwa vikosi vilivyopanda mlima Kilimanjaro kuudhibiti moto huo ni pamoja na vya Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Uhamiaji, Jeshi la Akiba, askari wa Tanapa, wadau wa utalii pamoja na wananchi.
Moto huo ulianza kuwaka katika eneo la karanga kuelekea Baranco mita 3,963 kutoka usawa wa bahari Oktoba 21, 2022, mpaka sasa hakuna madhara ya kibinadamu yaliyojitokeza na shughuli za utalii zinaendelea kama kawaida.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika lango la Mweka muda mfupi kabla ya kuanza safari kuelekea eneo la tukio kuuzima moto, Profesa Sedoyeka amesema wameendelea kuongeza nguvu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na kwamba mpaka jioni kutakuwa na mafanikio makubwa.
"Mpaka sasa angalau tumeweza kuzima moto kwa baadhi ya maeneo kwa kusaidiana na wananchi na mpaka asubuhi kulikuwa na mafanikio makubwa ya jitihada za kuzima moto katika maeneo ya Karanga ambapo ndio moto ulipoanzia"
"Licha ya kwamba tumeweza kudhibiti moto usisambae maeneo mengi kuna baadhi ya maeneo moto bado upo ila kuna eneo moja la upande wa Mweka lina moto na timu zote zipo pale na sisi tunakwenda kuongeza nguvu na tunategemea mpaka jioni tutakuwa na mafanikio makubwa zaidi,"
Katibu mkuu huyo ameongozana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Seleman Jafo kwenda kushirikiana na wadau kuuzima moto huo ambapo amesema atakuwepo hadi watakapofanikiwa kuukabili moto huo.
Baadhi ya wadau wa utalii wamejitokeza kushirikiana na Serikali katika kuongeza nguvu ya kuuzima moto huo pamoja na kutoa misaada ya vyakula kwa ajili ya vijana waliopanda mlima Kilimanjaro kukabiliana na moto huo.
Katibu wa Jumuiya ya Makalasinga Mjini Moshi, Navraji Bhamra asema kama wadau wa sekta ya utalii nchini wameamua kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine kuhakikisha wanatumia nguvu zote kuudhibiti moto huo.
Naye Romel Mosha wa kampuni ya utalii ya Kilimandscharo Active, ambaye ametoa vijana 20 na kuwagharamia kupanda mlima kuzima moto, amesema jitihada za kuuzima moto huo zinahitajika na ni jukumu la kila Mtanzania kwa Kuwa mlima huo ni urithi wa dunia.