Puma Energy watoa mafuta bure kwa wanawake

Muktasari:

  • Wakati dunia ikiadhimisha siku ya wanawake kampuni ya mafuta ya Puma Energy imeadhimisha siku hiyo  kutoa mafuta kwa wanawake wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi wakiwemo walemavu wanaoendesha bajaji.

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha siku ya wanawake kampuni ya mafuta ya Puma Energy imeadhimisha siku hiyo  kutoa mafuta kwa wanawake wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi wakiwemo walemavu wanaoendesha bajaji.

Hatua hiyo imefikiwa ili kuwapongeza wanawake hao kwa jitihada zao licha ya changamoto lukuki wanazokabiliana nazo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Meneja rasilimali watu wa Puma Energy kwa Bara Afrika,  Loveness Hoyange amesema  kampuni hiyo inatambua namna wanawake hao wanavyochakarika katika harakati za ujenzi wa Taifa.

“Tunatambua namna gani wanawake siku hizi wanajituma, mfano hawa wenye ulemavu hawajachukulia hali yao kuwa sababu ya kujibweteka wanafanya kazi inayowawezesha kuendesha maisha.”

“Kwa kuliona hilo kampuni yetu imeamua kuwapatia mafuta ili nao waweze kusherehekea siku hii ya wanawake kwa pamoja tukiwashukuru kwa mchango wao katika sekta ya usafirishaji,” amesema Loveness.

Naye meneja wa operesheni wa Puma Energy,   Lameck Hiliyai amesema kampuni hiyo inathamini mchango wa wanawake katika jamii na inafanya kila jitihada kuhakikisha kunakuwa  na uwiano unaoridhisha wa wanawake na wanaume ndani ya kampuni.

Jasmine Milanzi, dereva wa bajaji amesema jamii inapaswa kuwathamini wanawake wenye ulemavu licha ya changamoto lakini wanaingia ulingoni kupambana.

“Mimi ni mlemavu wa viungo, sijalemaa akili nimetafuta namna yangu ya kupambana ndio kama hivi nasomesha watoto, nina sehemu ya kuishi na maisha yangu ya kila siku yanakwenda. Watu wakituona walemavu wasifikiri hatuwezi kufanya chochote,” amesema Jasmine.

Kwa upande wake mwanamuziki Judith Wambura ‘Jide’ ambaye ni mmoja waliopata zawadi ya mafuta aliwataka wanawake kutokata tamaa na kusimamia ndoto zao.

“Nimeona wanawake siku hizi wanapambana niwasihi hakuna kurudi nyuma, simamia ndoto yako na usikubali mtu akuyumbishe wala kukukatisha tamaa, hakuna asichoweza kufanya mwanamke, tusichague kazi.”

“Hatuna sababu ya kuhofia na jamii itambue kuwa mwanamke anaweza hivyo inapotokea nafasi na ana vigezo vya kuitumikia basi apewe bila kuwepo milolongo,” amesema.