Puma kuanzisha vituo vipya vya mafuta Tanzania

Thursday April 29 2021
By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Katika kuunga mkono lengo la Serikali la kuanzisha na kuendeleza viwanda, kampuni ya mafuta ya Puma Energy imejipanga kuanzisha vituo vipya vya mafuta mwaka 2021.

Mafuta ni nishati  muhimu kwa shughuli za usafirishaji wa bidhaa, rasilimali watu na uendeshaji wa mitambo inayotumika viwandani.

Hadi kufikia jana Jumatano Aprili 28, 2021 kampuni hiyo imeanzisha vituo vipya 10 katika Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kagera na Morogoro.

Meneja wa mauzo ya rejareja wa kampuni hiyo, Vennesy Chilambo ameeleza kuwa pamoja na kupanua wigo wa biashara mpango huo unalenga kuhakikisha ubora wa mafuta yanayotumika kwenye mnyororo mzima wa uendeshaji wa viwanda na usafirishaji nchini.

Katika kutekeleza hilo Vennesy amesema kuanzia sasa vituo vyote vya kampuni hiyo nchi nzima vitatoa huduma kwa saa 24.

Amebainisha kuwa kampuni hiyo inatambua inahitajika kusaidia jamii kwa kuhakikisha kuna upatikanaji wa mafuta na vilainisho kwa gharama nafuu na ubora unaokidhi viwango.

Advertisement

“Rais amesema kazi iendelee na sisi tunaungana naye kuhakikisha huduma zetu zinawafiki watanzania wengi ili wafanye kazi.”

“Kama inavyofahamika ubora wa bidhaa zetu, tunataka isiishie mijini pekee tunazidi kusogea katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kuwafikia watumiaji wa vyombo vya moto,” alisema Vennesy.

Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) Godfrey Chibulunji alisema mamlaka hiyo imeandaa kanuni zinazotoa mwongozo kwa kampuni zote za mafuta nchini kuwa na vituo vijijini.

Alisema lengo ni  kukabiliana na madhara yanayojitokeza kutokana na watu hasa maeneo ya vijijini kuhifadhi majumbani petroli na dizeli kwa ajili ya biashara na matumizi.

Hali hiyo inatokana na kukosekana kwa vituo vya mafuta katika  vijijini na kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata mafuta.

Advertisement