Q Chief amuomba radhi Diamond

Q Chief amuomba radhi Diamond

Muktasari:

  • Abubakar Katwila maarufu Q Chief amewaomba radhi mashabiki na wadau wa muziki nchini Tanzania kwa kutoa lugha chafu dhidi ya msanii mwenzake, Nassib Abdul ‘Diamond Platnumz’ na meneja wa mkali huyo wa wimbo wa Waah, Sallam Sharaf.


Dar es Salaam. Abubakar Katwila maarufu Q Chief amewaomba radhi mashabiki na wadau wa muziki nchini Tanzania kwa kutoa lugha chafu dhidi ya msanii mwenzake, Nassib Abdul ‘Diamond Platnumz’ na meneja wa mkali huyo wa wimbo wa Waah, Sallam Sharaf.

Mwanzoni mwa Februari 2021 video zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii Q Chief akionekana kutoa lugha chafu dhidi ya wawili hao akiwatuhumu kutumia picha yake kwenye bango linaloonyesha orodha ya wasanii watakaotumbuiza kwenye shoo ya Wasafi Tumewasha iliyofanyika jijini Dar es Salaam Januari 31, 2021.

Alilalamika kuwa licha ya picha yake kuonekana hakuwa akilifahamu tamasha hilo na wala hakualikwa.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi Februari 27, 2021, msanii huyo aliyetamba zaidi mwanzoni mwa miaka ya 2000 amesema alichukizwa na jambo hilo na hasira ndio zilimfanya kutoa lugha chafu.

"Mimi sina mbawa ni binadamu wa kawaida kwa hiyo nakasirika, nachukia na naumia mtu anaponifanyia mambo ambayo siyapendi.”

"Tuliwaandikia barua ya kisheria na wameijibu juzi lakini nisingependa kusema wametujibu nini kwa sababu ni suala lililopo mikononi mwa vyombo vya dola kwa sasa,” amesema akisisitiza kuwa kuomba radhi haimaanishi ameacha kufuatilia jambo hilo.