Raia wa Burundi wazidi kujiandikisha kurejea kwao

Mkuu wa wilaya ya Kakonko, kanali Hosea Ndagala akizungumza leo katika mkutano na wakimbizi kutoka Burundi kwenye kambi ya Mtendeli iliyopo wilayani humo mkoa Kigoma, Picha na Happiness Tesha.

Muktasari:

  • Utaratibu wa kuwarejesha wakimbizi kwa hiari tangu ulipoanza mwaka 2017  hadi kufikia Aprili 2021 raia  116,652 wa Burundi wamerejea katika nchi hiyo wakitokea Tanzania huku 144,791 wakitajwa kubaki katika kambi mbalimbali.

Kakonko. Utaratibu wa kuwarejesha wakimbizi kwa hiari tangu ulipoanza mwaka 2017  hadi kufikia Aprili 2021 raia  116,652 wa Burundi wamerejea katika nchi hiyo wakitokea Tanzania huku 144,791 wakitajwa kubaki katika kambi mbalimbali.

Akizungumza leo Jumatano Aprili 14, 2021 na wakimbizi wanaoishi kambi ya Mtendeli wilayani Kakonko mkoani Kigoma mratibu wa wakimbizi Kanda, Nashon Makundi amesema uandikishaji na kurejea kwa wakimbizi hao umekuwa ukisuasua kwa kambi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu.

Amebainisha kuwa kuna baadhi ya watu wachache wamekuwa wakipita katika kambi hiyo na kuwahamasisha wakimbizi hao wasirejee nchini kwao jambo alilodai kuwa halikubaliki kwani wanatakiwa kurudi kwenda kujenga nchi yao.

 Amesema baadhi ya wakimbizi wana hofu kwamba wakirudi nchini mwao maisha yatakuwa magumu akiwataka kuishinda hofu.

"Hofu ni tabia ya mwanadamu na ni kikwazo cha maendeleo, mjitokeze kwa wingi kujiandikisha na kurejea nchini kwenu kwani bado Taifa linawahitaji ili mlitumikie, wengi wenu hapa mna nguvu nyingi na afya nzuri," amesema Makundi.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema atafurahi endapo wakimbizi hao wakirudi makwao na kurudi Tanzania kwa kufuata utaratibu.

"Mmekaa sana hapa Kigoma mmeona fursa mbalimbali, nendeni nyumbani mkawaambie na wengine mje kuwekeza kwa kufuata utaratibu, tunawakaribisha na tunawapenda kwani nyinyi ni ndugu zetu na majirani zetu wa hali zote," amesema Andengenye.