Raila, Ruto vita yahamia bungeni

Muktasari:

  • Baada ya kushindwa mahakamani, Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya unaongozwa na Raila Odinga, umehamishia vita mpya katika kuwania kuongoza mhimili wa Bunge kwa kumteua Kalonzo Musyoka kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la 13.

Nairobi. Baada ya kushindwa mahakamani, Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya unaongozwa na Raila Odinga, umehamishia vita mpya katika kuwania kuongoza mhimili wa Bunge kwa kumteua Kalonzo Musyoka kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la 13.

Bunge la Kenya ni mhimili unaojitegemea kama ilivyo Mahakama na ndio linalopitisha kwa mujibu wa Katiba uteuzi wa baadhi ya viongozi unaofanywa na Rais.

Hayo yanajiri baada ya Muungano wa Azimio kushindwa mahakamani kwenye kesi ya kupinga ushindi wa urais wa kiongozi wa United Democratic Alliance (UDA), Dk William Ruto, ambaye ndiye Rais mteule wa tano wa Kenya.

Kalonzo alizaliwa Desemba 24, 1953 ni kiongozi wa Chama cha Wiper na amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwamo makamu wa rais wakati wa utawala wa Rais Mwai Kibaki.

Pia, mchuano wa nafasi hiyo unakuja wakati Spika wa Bunge lililopita, Justin Muturi wa Chama cha Democratic amejiunga na Muungano wa UDA akishiriki kumbeba Dk Ruto.
Bado haijaelezwa kama Muturi atagombea tena nafasi hiyo, lakini UDA kimevuna wabunge 159 huku Azimio wakiwa na wabunge 162.

Hata hivyo, kuna wabunge 10 walioingia bungeni kwa njia ya wagombea binafsi.
Lakini, Agosti 17, 2022 Dk Ruto baada ya kutangazwa mshidi wa urais, alisema wabunge hao 10 wametangaza kujiunga na UDA, hivyo anaweza kuwa na wabunge 169.

Vita kubwa kwa Azimio na UDA itahamia katika kuwashawishi wabunge 10 kuwaunga mkono kwenye mbio za uspika.
Tayari Rais anayeondoka madarakani Uhuru Kenyatta ametangaza kwenye gazeti la Serikali kwamba Bunge la 13 litaanza kesho kwa kumchagua Spika wa Bunge.

Safari yake kwenye siasa
Kalonzo ana nafasi nzuri ya kuchaguliwa kuwa spika kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu katika sheria na siasa za Kenya.
Wakili huyo aliwahi kuwa naibu spika wa Bunge la Kitaifa kati ya mwaka wa 1988 na 1992 wakati wa utawala wa Kanu.
Katika uchaguzi uliopita, Raila aliahidi kumteua Kalonzo kwenye nafasi ya waziri mkuu aliyotaka kuiunda endapo angeshinda urais.
Kalonzo alijiunga na siasa ndani ya Kanu na alichaguliwa mbunge mara ya kwanza mwaka 1985 na mwaka 1986 aliteuliwa kuwa naibu waziri kwenye wizara ya kazi za umma.