Raila sasa kuamua kati ya Kalonzo, Karua au Kenneth

Saturday May 14 2022
railapiic
By Luqman Maloto

Mgombea urais wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga, sasa anapaswa kuchagua kati ya majina matatu, Kalonzo Musyoka, Martha Karua na Peter Kenneth, mmoja awe mgombea mwenza wake.

Jopo la kuchakata jina la mgombea mwenza wa Raila, lilikamilisha kazi yake na kuwasilisha mapendekezo kwa mgombea urais. Kazi kwa Raila kuchagua mmoja.

Mkuu wa jopo hilo, Noah Wekesa aliviambia vyombo vya habari Nairobi kuwa majina yaliyopendekezwa ni siri na Raila ameshakabidhiwa kulingana na utaratibu.

Martha ambaye ni Kiongozi wa Narc-Kenya, ndiye mwanamke pekee kati ya waliopendekezwa. Kalonzo ambaye ni Makamu wa Rais wa zamani na Kenneth aliyepata kuwa mbunge wa Gatanga, wote ni wanaume.

Mei 16, mwaka huu ni ukomo wa kila mgombea urais kuwasilisha jina la mgombea mwenza. Hivyo, Raila anapaswa kufanyia kazi majina hayo na kuchagua moja kabla ya tarehe ya ukomo.

Kwa mujibu wa Wekesa, majina yaliyopendekezwa yameambatanishwa na sifa, vilevile vigezo ambavyo jopo lilizingatia kupata viongozi hao watatu ambao wameonekana wanafaa kuwa naibu rais kama Raila atashinda urais.

Advertisement

“Vigezo vyote vilipimwa kwa kutazama sifa zilizotajwa kwenye Katiba, uelewa wa Serikali, wajihi wa mgombea, uwezo wa kisiasa, utiifu, mikakati, mapambano ya rushwa na kadhalika,” alisema Wekesa.

Seneta wa Kitui, Enoch Wambua ni mjumbe wa jopo la kuchakata jina la mgombea mwenza, akitokea kambi ya chama cha Wiper, kinachoongozwa na Kalonzo. Wambua hakuwepo kwenye mkutano na wanahabari ingawa alisema ni sehemu ya uamuzi uliofanyika.

Awali, Wambua alilalamika kuwa alikuwa akitengwa na wajumbe wengine wa kamati hiyo, hivyo kutishia kujitoa. Chama cha Wiper pia kimekuwa kikitishia mara kwa mara kujiondoa Azimio la Umoja One Kenya kwa hoja kuwa wanatengwa na hawatendewi haki.

Upande wa Wekesa, alisema wakati wa kuzungumza na waliopendekezwa, kila mgombea aliulizwa uelewa wake kuhusu masuala nyeti yanayoikumba Kenya hivi sasa na mapendekezo yao kuhusu nini ambacho Serikali itakayoundwa na Azimio itatakiwa kufanya ikishachukua ofisi.

“Msisitizo zaidi ulikuwa je, mgombea anachagulika? Uwezo wa kuhamasisha kura, je, ni kiongozi mwanamabadiliko? Ni mtu wa kutegemewa au tegemezi? Ana uvumilivu wa kisiasa? Ana maarifa ya kisiasa kwenye uchaguzi?” alihoji Wekesa.

Akifafanua zaidi, Wekesa alisema wajumbe wote saba wa kamati ya uteuzi wa jina la mgombea mwenza wa Azimio la Umoja One Kenya, walishiriki kufanikisha mchakato wote.

“Uamuzi wa mwisho ulifikiwa kwa kupima wastani wa mchango wa kila mmoja katika jopo letu,” Wekesa alitoa ufafanuzi huo kwa vyombo vya habari.

Ukiwaacha Martha, Kenneth na Kalonzo ambao majina yao yamepelekwa kwa Raila kungoja uamuzi wa mwisho, wengine walioitwa na kamati kufanyiwa usaili ni Naibu Kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) Karua, Kenneth na Musyoka, Hassan Joho na bosi mwingine wa ODM, Wycliffe Oparanya.

Bosi mwingine wa Narc Kenya, Charity Ngilu, Waziri wa Kilimo, Peter Munya, akitokea Chama cha National Unit (PNU), mwakilishi wa wanawake jimbo la Murang’a, Sabina Chege, Kiongozi wa Chama cha National Liberal (NLP), Stephen Tarus na Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui, kutoka Ubuntu Peoples’ Forum (UPF). Wote hao walifanyiwa usaili.

Mwenyekiti wa chama Kenya African National Union (Kanu), Gideon Moi, ambaye alikuwa kati ya majina yaliyopenya kwenye mchujo wa awali, alijitoa kwa hoja kwamba anampendekeza Kalonzo kuwa mgombea mwenza anayefaa kusimama na Raila.

Jumapili iliyopita, Kalonzo alikuwa na mkutano wa hadhara Kaunti ya Makueni, Ukambani. Na matarajio yalikuwa Raila angejumuika naye. Hata hivyo, Waziri Mkuu huyo wa zamani hakutokea.

Sintofahamu ilikuwa kubwa kwa kitendo cha Raila kumkwepa Kalonzo na mkutano wake, kwa sababu inanong’onwa ndani ya Azimio la Umoja kuwa nafasi ya mgombea mwenza ni ya Rais Uhuru Kenyatta na chama chake, Jubilee.

Hivi karibuni, ilitolewa taarifa kuwa majina 20 yalipendekezwa kwenye jopo maalumu lililoundwa na Baraza la Azimio. Majina hayo hatimaye yamechujwa mpaka kupatikana matatu. Sasa anasubiriwa Raila aamue.

Na katika majina yaliyopendekezwa, ilielezwa Uhuru alitoa mapendekezo mawili; jina la kwanza likiwa la mbunge wa zamani wa jimbo la Gatanga, Peter Kenneth na mwakilishi wa wanawake jimbo la Murang’a, Sabina Chege.

Raila alitaka kusimama na Gavana wa Mombasa anayemaliza muda wake, Hassan Joho. Kwa vile Joho hayumo katika majina matatu yaliyopendekezwa, haijulikani upi utakuwa msimamo wa kiongozi huyo wa ODM. Ataheshimu mapendekezo ya kamati?

Upande wa Uhuru, bado jina la mtu aliyempendekeza kwa nafasi ya kwanza yumo. Ni Kenneth. Inaelezwa kuwa kama Kenneth atapitishwa kuwa mgombea mwenza, Uhuru atapata mwanya mzuri wa kumuuza Raila eneo la Mlima Kenya ambalo lina utajiri mzuri wa kura.

Advertisement