Rais afuta mapori 12 na kuwapa wananchi

Muktasari:

  • Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya Makazi, Dk Angella Mabula amesema Rais Samia Suluhu Hassan amefuta mapori 12 nchini ili kuwapa wananchi.

Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maendeleo ya Makazi, Dk Angella Mabula amesema Rais Samia Suluhu Hassan amefuta mapori 12 nchini ili kuwapa wananchi.

Dk Mabula ameyasema hayo leo Ijumaa, Juni 23 wakati akichangia mjadala wa bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/2023.

Amesema kamati ya mawaziri wanane imefikia mikoa 12 kati ya 26 nchini na kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kufutwa kwa mapori 12 ili kuwapa wananchi.

“Tumefikia vijiji 412 kati ya 920 ambavyo wananchi wanakwenda kukaa. Ninajua katika uwekezaji na utalii watu watakwenda huko na kama kuna migogoro ya mipaka ni wazi hakutakuwa na mazingira mazuri katika kupokea,” amesema.

Kuhusu mipango miji, Dk Mabula amesema watahakikisha wanafuatilia halmashauri kuhakikisha kuwa inakuwa na mipango ya matumizi ya ardhi na kutenga maeneo ya uwekezaji.

Amesema wametenga Sh50 bilioni ambazo zitakopeshwa kwa halmashauri kwa ajili ya kupanga matumizi ya ardhi.