Rais Magufuli ahimiza Watanzania kulima mazao ya chakula kuzisaidia nchi zilizoathirika kwa corona

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewataka Watanzania kulima mazao mbalimbali hasa ya chakula kwa ajili ya kuzisaidia nchi ambazo zinashindwa kufanya uzalishaji kwa sababu watu wake wamefungiwa majumbani ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona (Covid-19).

Rais Magufuli ametoa rai hiyo leo Januari 17 kwenye ibada ya misa Takatifu katika kanisa katoliki la Bikira Maria, Parokia ya Chato. Ibada hiyo iliongozwa na paroko wa parokia hiyo, Padre Henry Mulinganisa.

Katika ibada hiyo, Rais Magufuli amewataka waumini wa kanisa hilo kuendelea kumtukuza na kumshukuru Mungu kwa Baraka zake kwa Taifa hasa kwa kuliepusha na janga la ugonjwa wa corona (Covid-19) wakati ugonjwa huo ukisababisha vifo vya maelfu katika mataifa mengine.

“Sasa hivi mvua zinanyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, nawaombeni sana ndugu zangu Watanzania tulime mazao hasa ya chakula, tulime kwa wingi ili baadaye tuje kuwasaidia wenzetu ambao wanashindwa kulima kutokana na corona,” amesema Rais Magufuli. 

Rais Magufuli ambaye pia aliambatana na mke wake, Janeth Magufuli katika ibada hiyo, amewapongeza waumini wa kanisa hilo kwa kufanikisha upanuzi wa kanisa lao ambalo sasa lina nafasi ya kutosha waumini wengi zaidi kufanya ibada kwa wakati mmoja.