Rais Magufuli kasema, mnasubiri nini kuvaa barakoa?

Rais Magufuli kasema, mnasubiri nini kuvaa barakoa?

Muktasari:

  • Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa nyakati tofauti wamevunja ukimya kuhusu matumizi ya barakoa katika kujikinga na maambukizo ya maradhi ya kupumua, hivyo ni wajibu wetu sasa kuamua baina ya kifo na uhai.

Rais Magufu Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa nyakati tofauti wamevunja ukimya kuhusu matumizi ya barakoa katika kujikinga na maambukizo ya maradhi ya kupumua, hivyo ni wajibu wetu sasa kuamua baina ya kifo na uhai.

Ninasema hivyo kwa sababu kabla ya kauli za viongozi hao, kulikuwa na minong’ono kuwa pengine wakubwa hao walikuwa wamezuia matumizi ya barakoa kama njia mojawapo iliyopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Pamoja na njia nyingine za kujikinga na maambukizo ya ugonjwa huu, WHO ilielekeza watu kuepuka kusongamana, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka au kutumia vitakasa mikono na kuvaa barakoa.

Ingawa hakuna kiongozi wa Kiserikali aliyetamka wazi kuwa Tanzania ina ugonjwa wa Uviko-19 au Covid-19, lakini kwa kauli na matendo ya viongozi wetu wakuu akiwamo Rais, ni dhahiri janga hili linaitikisa dunia na Tanzania pia.

Minong’ono ilikuwa mikubwa pale Rais alipoonekana kwenye matukio ya kitaifa akiwa hajavaa barakoa na kutotaja neno barakoa tangu Desemba 2020, hadi Jumapili Februari 21, kwamba pengine kuna katazo la kuvaa barakoa.

Lakini aliyekuwa wa kwanza kuvunja ukimya wa minong’ono hiyo ni Waziri Mkuu, Majaliwa wakati wa maziko ya aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, pale alipowaambia waombolezaji kuwa uvaaji barakoa haujakatazwa.

Nikimnukuu alisema: “Barakoa utaivaa pale ambapo unajua shughuli zako za siku hiyo zitakupelekea kupata huduma au kutoa huduma na mwingine ndani ya umbali wa chini ya mita moja na kusema hakuna aliyekataza uvaaji wa barakoa.”

Kauli ya Waziri Mkuu ikafanana na aliyoitoa Rais Jumapili, Februari 21, 2021 wakati wa Ibada ya Dominika ya Kwanza ya Kwaresima iliyofanyika Kanisa la Mtakatifu Petro Jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Padri Alister Makubi.

“Sijasema msivae barakoa wala msini quote (msininukuu) vibaya, lakini kuna barakoa nyingine sio nzuri. Nataka niwaambie huu ndio ukweli. Utaletewa barakoa nyingine ambazo zitawaletea matatizo,” alisema Rais Magufuli.

“Ukitaka kuvaa barakoa, vaa zilizotengenezwa na Wizara ya Afya, MSD (Bohari kuu ya Dawa), wanatengeneza barakoa ukishindwa shona yako mwenyewe, kachukue likitambaa hata kama ni kanga likunje hata mara tano,” alisisitiza Rais.

Kauli za viongozi hao wawili ukizifanyia uchambuzi, utagundua kuwa kulikuwa na maneno kuwa pengine wamezuia uvaaji wake na ndiyo maana Rais na waziri mkuu katika matamshi yao wanasisitiza hakuna aliyekataza uvaaji wa barakoa.

Ninaamini baada ya kauli hii ya Rais, ni wajibu sasa wa Wizara ya Afya kubeba jukumu la kutoa elimu zaidi ya uvaaji sahihi wa barakoa na ni wakati wa viongozi wa kisiasa na wataalamu kuonyesha njia badala ya kusubiri bendera fuata upepo.

Ninaipongeza Wizara ya Afya kwamba baada tu ya Rais kutamka neno barakoa, nao katika taarifa yao wakaitaja sasa kama moja ya njia za kujikinga na maambukizo hayo, baada ya kulikwepa kwa karibu miezi miwili mfululizo.

Tupende tusipende, tukubali tusikubali, janga la corona utatuzi wake lazima uegemee katika sayansi na ushahidi kupitia tafiti na haina maana siabudu tiba mbadala, hapana, ila ni lazima ziwe zile zilizofanyiwa tafiti kisayansi.

Nasema hivyo kwa kuwa kisayansi hakuna tiba ya ugonjwa unaosababishwa na virusi kama vya corona, bali kuna chanjo, hivyo basi tuzingatie maelekezo ya WHO na maelekezo yaliyo sahihi ya wataalamu wetu ya njia sahihi za kujikinga.

Sasa kwa kuwa Rais na waziri mkuu wetu na viongozi wengine wamehitimisha minong’ono ya imekatazwa au haijakatazwa, huu ni wakati sasa wa kila mmoja wetu kurudi kwenye mstari kuanzia kwenye usafiri wa umma hadi masokoni.

Ni lazima Watanzania wajue katika mkusanyiko wowote, hatakutana na mtu mwenye alama usoni kuwa ana maambukizo ya virusi vya corona, ni wajibu wake kumuona kila ambaye yuko karibu naye umbali chini ya mita moja ana corona.

Kama nilivyotangulia kusema, kama Rais Magufuli kasema barakoa ni ruksa na akatoa aina ya barakoa ambazo ni salama kwa Watanzania, wewe ni nani usubiri hadi uchapwe viboko ndiyo uvae? Jilinde wewe, mwenzako na familia yako.

Haitakuwa na maana kama unanawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, kutumia vitakasa mikono lakini unaingia ndani ya basi unasafiri kwa saa 8 na ndani ya basi mko zaidi ya 40 wote hamjavaa barakoa, mnapumuliana virusi. Chukua hatua.

0769600900