Rais Mwinyi atoa wito wa kumuenzi hayati Karume

Muktasari:

Katika hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud wakati wa Kongamano la tatu la kumbukumbu ya Hayati Karume lililoandaliwa na Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Zanzibar, Rais amesema Karume anapaswa kuenziwa kwa vitendo.

Unguja. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amesema wakati wa kipindi hiki cha kuadhimisha miaka 49 ya muasisi wa Taifa hilo Hayati Abeid Aman Karume anapaswa kuenziwa kwa kusimamia tunu alizoziamini.


Ametoa kauli hiyo leo Aprili 12 katika hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud wakati wa Kongamano la tatu la kumbukumbu ya Hayati Karume lililoandaliwa na Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Zanzibar jana.


"Kimsingi tunastahili kumuenzi kwa vitendo na  maisha yetu yote yaweze kuhakisi tabia zake, katika utawala wake aliimba upendo na umoja wa taifa, msingi bora ya uchumi, kuleta haki na kupambana na dhuluma," amesema


Amesema kongamano hilo linamkumbusha kila mmoja kwa nafasi yake kurejea katika misingi ya falsafa ya uwazi, uadilifu, ushirikishwaji, upendo amani na uadilifu tunu alizoziishi Mzee Karume katika maisha yake na katika ujenzi wa Zanzibar.


"Kwahakika tunaweza kupata matokeo makubwa kila mmoja wetu katika utendaji na utekelezaji wa sera mbalimbali za serikali katika misingi ya falsafa hizo,
“Tukizingatia tunu hizi alizoziishi tutaweza kubadili fikra zetu na mienendo yetu na kuleta utendaji bora wenye kuboresha maisha ya wananchi wetu"


Pia alisema wakati wa kuadhimisha miaka 49 bila kuwa na Mzee Karume kunatoa wasaa wa kurejea hekima  na busara zake kwa kujikumbusha misingi ya utendaji majukumu mbalimbali yenye kuacha alama katika  maisha ya watu.


"Tuendelee kukuza uzalendo, alikuwa mtu wa kupenda na kusaidia watu hizi ni sifa muhimu kwa kiongozi wa umma, tuna kila sababu kutembea kifua mbele kutokana na kazi kubwa alizoifanyia Zanzibar.


Naye Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Professa Shadrack Mwakalila alisema lengo la kongamano hilo ni mwendelezo wa kumuenzi katika fikra na falsafa zake ambazo bado zinaishi leo kwa kujikumbusha misingi mikubwa ya umoja na mshikamano.


Naye Mwenyekiti wa bodi ya chuo Steven Wasira amesema kwamba historia ya hayati Karume bado haijafahamika kwa wananchi wengi badala yake wengi wanamfahamu kama muasisi lakini bila kuingia ndani kuelezewa kwa kina