Rais Samia aagiza tozo za mafuta kupunguzwa

Rais Samia aagiza tozo za mafuta kupunguzwa

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameelekeza kupunguzwa kwa tozo zinazotozwa na Taasisi mbalimbali katika bidhaa za mafuta hapa nchini zenye thamani ya Sh102 bilioni kwa mwaka, kwa lengo la kupunguza bei za mafuta na kuwapa unafuu wananchi.


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameelekeza kupunguzwa kwa tozo zinazotozwa na Taasisi mbalimbali katika bidhaa za mafuta hapa nchini zenye thamani ya Sh102 bilioni kwa mwaka, kwa lengo la kupunguza bei za mafuta na kuwapa unafuu wananchi.

Rais Samia ametoa agizo hilo  leo Jumanne Oktoba 5 , 2021 wakati akipokea taarifa kutoka kwa Waziri wa Nishati, January  Makamba kuhusu utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa Wizara hiyo kupitia mwenendo wa biashara ya mafuta na bei zake hapa nchini.

Taarifa iliyotolea na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Jaffar Haniu imeeleza kuwa utekelezaji wa maagizo hayo unaenda sambamba na marekebisho ya kanuni mbalimbali zinazohusiana na tozo na kuchapishwa katika gazeti la Serikali leo Oktoba 05 ,2021.

Katika taarifa hiyo imeeleza kuwa Rais Samia amechukua hatua ili kukabiliana na upandaji wa bei za mafuta katika soko la dunia, ambapo kwa muda mrefu imekuwa ikipanda kwa kiwango kikubwa na kuathiri watumiaji wa bidhaa hiyo hapa nchini.

“Taasisi zinazoguswa na maelekezo haya ni, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (tozo ya udhibiti), Mamlaka ya Bandari (tozo ya miundombinu), Mamala ya Mapato Tanzania (tozo ya kuchakata taarifa), Shirika la Viwango Tanzania (tozo ya kupima ubora wa mafuta kwenye meli na gharama ya uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta),”

Taasisi nyingine Wakala wa Vipimo Tanzania (tozo ya uhakiki wa ujazo wa mafuta melini), Wakala wa Usimamizi wa Meli (tozo ya forodha) na Mamlaka ya Serikali  za Mitaa (ushuru wa huduma kwenye Halmashauri nne zenye maghala ya kupokea mafuta kwa jumla).  Halmashauri hizo ni Kigamboni na Temeke za Jijini Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.

Aidha, Rais Samia pia ameagiza ufanyike mchakato wa haraka wa kupeleka marekebisho ya Sheria Bungeni zinazohitaji marekebisho ya haraka katika kukabiliana na kupanda kwa bei za mafuta  hapa nchini,  ili kumlinda mtanzania na gharama za maisha zinazotokana na  kupanda kwa bei ya mafuta.

Katika mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Nishati January Makamba, Waziri wa Fedha na Mipango  Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo,  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Ummy  Mwalimu.

Wengine ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato, Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Eliezer Feleshi, Katibu Mkuu Wizara ya Niashati Leonard Masanja, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Kheri Mahimbali  na watendaji wa Taasisi mbalimbali.