Rais Samia aahidi ujenzi kiwanda cha parachichi Iringa

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Kutokana na kushamiri wa kilimo cha zao la Parachichi, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameahidi ujenzi wa kiwanda cha kuchakata zao la Parachichi Mkoani Iringa.

Iringa. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameahidi ujenzi wa kiwanda cha kuchakata parachichi katika mkoa wa Iringa ili kuliongezea thamani zao hilo.

 Akizungumza na wananchi wa eneo la Nyololo baada ya kuanza ziara yake ya siku tatu mkoani Iringa, leo Alhamisi Agosti 11, 2022 akitokea Mkoa wa Njombe, Raisi Samia amesema kiwanda hicho kinajengwa kutokana na maombi aliyokuwa amepewa.

“Najua Iringa na Njombe ni wakulima wa maparachichi, kile kiwanda ambacho mbunge aliomba kisimamishwe kinabaki hapa. Na kule Njombe wameomba cha kwao tutawajengea,” amesema Rais Samia.

Amesema lengo ni kusafirisha zao hilo nje ya nchi likiwa limeongezewa thamani.

“Lengo ni kusafirisha maparachichi mengi zaidi yenye hadhi nzuri ili tupate pesa nyingi zaidi,” amesema Rais Samia.

Baadhi ya wakulima wa parachichi wamesema ujenzi wa kiwanda hicho utaondoa hofu ya kukosekana kwa soko la zao hilo hapo baadae.

Amesema, kutokana na muamko mkubwa wa wakulima wengi kuwekeza kwenye zao hilo, walikuwa na hofu ya kuja kuyumba kwa soko siku za usoni.

“Kama kiwanda kitajengwa kilimo cha zao hili kitaendelea kustawi, binafsi niliogopa labda lingekuja kuyumba kwa sababu kila mtu analima parachichi. Tunashukuru kwa ahadi hii,” amesema Inocent Kalinga, mkulima wa Parachichi wilayani Mufindi.