Rais Samia aeleza Anna Mkapa alivyomuingiza katika siasa

Rais Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amebainisha kwamba Anna Mkapa, mke wa Rais mstaafu, Hayati Benjamin Mkapa, ndiye aliyemfanya aingie kwenye siasa.


Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amebainisha kwamba Anna Mkapa, mke wa Rais mstaafu, Hayati Benjamin Mkapa, ndiye aliyemfanya aingie kwenye siasa.

Rais Samia amebainisha hayo leo Jumatatu Juni 27 jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha kilele cha maadhimisho ya miaka 25 ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Fursa Sawa Kwa Wote (EOTF) ulioanzishwa Juni 1997.

Amesema alipokuwa kwenye shughuli moja ya EOTF, aliachwa na gari alilokwenda nalo, Mama Anna Mkapa alimwona amesimama akamwambia aingie kwenye gari lake.

Amesema akiwa kwenye gari lake Mama Anna alimwambia aingie kwenye siasa kwa sababu anamwona ana uwezo. Amesema maneno hayo yalimwingia na ulipofika msimu wa uchaguzi mwaka 2000, alijitosa kwenye siasa akafanikiwa kushinda uwakilishi huko Zanzibar.

"Maneno ya Mama Mkapa mle kwenye gari ndio yaliyonipa nguvu ya kuingia kwenye siasa. Kwa hiyo na mimi nimepita kwenye EOTF, mnufaika pia wa Taasisi hii," amesema Rais Samia.

Amewataka wanawake kuendelea kujipanga na kuzalisha bidhaa bora kwa wingi kwa sababu masoko yapo na kwamba tayari baadhi yao wananufaika na matunda ya filamu ya Royal Tour kwa kuuza bidhaa zao kwenye mahoteli ambayo sasa yanajaa watalii.

"EOTF iendelee kuwajengea wanawake uwezo wa kibiashara kwa kushirikiana na Shirika la Viwango (TBS) na TanTrade. Nimekutana na mjasiriamali mmoja hapa, ameniambia tayari amepata mhuri wa TBS," amesema.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa EOTF, Mama Mkapa amesema taasisi yake ilianzishwa kwa lengo la kuiwezesha jamii kupiga vita ujinga, umasikini na maradhi.

Amesema EOTF iligawanya shughuli zake katika programu tatu ambazo ni kuwajengea wanawake na vijana uwezo wa kiuchumi, kutoa msaada wa kielimu kuanzia shule ya msingi hadi vyuo vikuu na kusaidia masuala ya afya.

"Katika kipindi hiki cha miaka 25, tumetoa mafunzo kwa wajasiriamali zaidi ya 6000 ambao nao wametengeneza ajira 65,000. Wameweza kutengeneza bidhaa zenye thamani ya Sh11 trilioni," amesema Mama Mkapa.


Kwa upande wa elimu, amesema watoto 1755 wamepatiwa msaada wa kielimu kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu na wengi wao sasa ni watumishi serikalini katika kada mbalimbali kama vile ualimu, udaktari na ngazi nyingine za uongozi.