Rais Samia aeleza umuhimu ujenzi kituo cha forodha
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza lengo la ujenzi wa kituo cha pamoja cha forodha kati ya Tanzania na Malawi ni kuhakikisha usalama wa watu na bidhaa zinazoingizwa nchini.
Kyela. Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza lengo la ujenzi wa kituo cha pamoja cha forodha kati ya Tanzania na Malawi ni kuhakikisha usalama wa watu na bidhaa zinazoingizwa nchini.
Rais Samia amesema hayo leo Jumapili Agosti 7, 2022 wakati akizindua mradi unaotekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) uliojengwa katika kata ya Njisi Kasumuru Wilaya ya Kyela ambao umefikia asilimia 87 .
Amesema lengo la ziara yake ya siku nne mkoani Mbeya ni kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali hususan kituo hicho na kuhimiza usalama wa watu na bidhaa uimarishwe sambamba na kuhakikisha bidhaa zinazoingizwa nchini zinalipiwa.
Samia amesema licha ya kuweka jiwe la msingi amefurahishwa na mapokezi ya wananchi wa Kyela na kutoa fursa kwa mbunge wa Kyela, Ally Mlaghila kueleza changamoto ili kuzitafutia majibu.
Akizungumza na Mamia ya wananchi wa Kyela, Mlaghila amemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia Sh800 milioni i kwa ajili ya mradi wa maji katika maeneo yenye changamoto.
Mlaghila alimuomba Rais kupitia mto Songwe unaotenganisha nchi ya Tanzania na Malawi, kuwepo kwa mradi wa kilimo cha umwagiliaji kutokana na changamoto za mafuriko zinazosababisha mpaka baina ya nchi hizo kutoeleweka .
''Mama tunaomba tusaidie mto huu utumike kuanzisha mradi wa kilimo cha umwagiliaji kwani yanapotokea mafuriko kuna shida sana kwa wananchi wangu makazi yao kuhama mara kwa mara mara kuwepo Tanzania mara Malawi," amesema.
Mtendaji nkuu wa Tanroad, Rogatus Mativila amesema mradi huo umekamilika kwa asilimia zaidi ya 87 licha ya kuwepo kwa changamoto huku akieleza kuwa chachu ya kukuza mapato ya serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amemuomba Rais Samia kusaidia kupatikana kwa gari la zimamoto kutokana na ukubwa wa mkoa huku akigusia kituo hicho kwamba kitaongeza mapato ya Serikali kutokana na watu wa nchi jirani ya Malawi kutegemea manunuzi ya bidhaa nchini Tanzania kwa kupitia mpaka wa Kasumuru Wilaya ya Kyela.
Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliwataka wananchi wa Kyela kujitokeza kwenye zoezi la sensa ya watu na makazi ili kumrahisishia Rais Samia katika kuboresha miradi ya maendeleo na mahitaji ya Watanzania.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Makame Mbarawa, amesema wamepokea maagizo yote yaliyotolewa na Rais Samia na yanaanza kufanyiwa kazi.
Mkazi wa Njisi Kasumuru, Johnson Ally ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kujenga kituo hicho kwani kitakuwa chachu ya kukuza uchumi kutokana na mwingiliano wa shughuli za kiuchumi.