Rais Samia afanya mazungumzo na Mjumbe wa Sudan Kusini

Rais Samia afanya mazungumzo na Mjumbe wa Sudan Kusini

Muktasari:

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo na Mjumbe maalum wa Rais wa Jamhuri ya Sudan ya Kusini, Salva Kiir Mayardit, Balozi Ayuel Aboung.

Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo na Mjumbe maalum wa Rais wa Jamhuri ya Sudan ya Kusini, Salva Kiir Mayardit, Balozi Ayuel Aboung.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Jumatano Septemba 15, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengi pia wameomba kutumia Bandari ya Dar es Salaam kusafirishia mizigo na kununua chakula kutoka Tanzania.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Aboung amesema pamoja na mambo mengine, Rais Salva Kiir Mayardit ametaka kuimarishwa zaidi kwa uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na Sudan Kusini.

Alitumia nafasi hiyo kueleza maombi ya Sudan Kusini kutumia Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo yake na pia kununua chakula kutoka Tanzania.


Pia Balozi Aboung amesema Sudan Kusini inaomba pindi reli ya kisasa (SGR) itakapokamilika itumie reli hiyo kusafirishia bidhaa zake.


“Lakini Sudani Kusini bado inahitaji kupata walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili kuanzia ngazi ya shule ya msingi kutoka Tanzania,” amesema.

Kwa upande wake Rais wa Tanzania, amemhakikishia mjumbe huyo kuwa Tanzania iko tayari kuendeleza ushirikiano uliopo kwa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili kwa manufaaya pande zote mbili.

“Kuhusu ombi la kutumia bandari ya Dar es Salaam, Tanzania iko tayari kushirikiana na Sudani Kusini katika kukuza uchumi wan chi zote mbili,” amesema Samia.