Rais Samia amteua Jenerali Mabeyo

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini (CDF), Jenerali Venance Mabeyo. Jenerali Mabeyo alifika Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumuaga Rais Samia jana Jumatano Juni 30, 2022. Picha na Ikulu

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais- Ikulu, Zuhura Yunus imesema kuwa uteuzi huo umeanzia leo Alhamisi Juni 30, 2022.

Uteuzi huo umekuja muda mfupi baada ya Mkuu huyo wa nchi kumuapisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) mpya, Jenerali Jacob Mkunda.

Wakati wa uapisho huo uliofanyika Ikulu ya Dar es Salaam, Rais Samia ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu alimshukuru huku akiahidi kumpangia majukumu mengine Mabeyo.

“Namshukuru Mungu kwa kumjalia Jenerali Mabeyo kumaliza kazi leo akiwa smart na bado ana nguvu. Nikushukuru Jenerali Mabeyo kwa kazi nzuri uliyofanya katika utumishi wako wa zaidi ya miaka 40 jeshini.

“Umefanya kazi yako kwa uadilifu mkubwa, umetumikia cheo chako kwa jitihada kubwa na umemaliza na kukabidhi kwa wengine. Tunakushukuru sana na tunakupongeza sana kwa sababu siyo kazi rahisi,” amesema Rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi aliahidi kuwa wataendelea kumteua katika majukumu mengine huku akisisitiza kwamba tayari Katibu Mkuu Kiongozi, Hussein Kattanga ameshampangia majukumu mengine.

“Unaacha ukiwa na nguvu, ukiwa bado kijana na kwa hiyo tutaendelea kukuteua, tutaendelea kukupa majukumu, uendelee kutusaidia.

“Nadhani jioni ya leo Katibu Mkuu Kiongozi atasikia kwenye bomba, tayari ameshakupangia kazi ya kufanya. Kwa hiyo tunakushukuru sana na tunakupongeza na tunakuomba bado uendelee kulitumikia taifa lako,” amesema Rais Samia.