Rais Samia amwapisha Mkuu wa Majeshi mpya, Mabeyo kupangiwa majukumu mengine

Rais Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Tanzania (CDF), Jenerali Jacob Mkunda katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Dar es Salaam leo Alhamisi Juni 30, 2022. Picha na Ikulu

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan amewapongeza pia viongozi wapya wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuwataka kwenda kuendeleza pale alipoishia Jenerali (mstaafu), Venance Mabeyo.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemwapisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob Mkunda huku akiahidi kumpangia majukumu mengine CDF aliyemaliza muda wake, Jenerali Venance Mabeyo.

Hafla ya la kumwapisha Jenerali Mkunda ilifanyika leo Alhamisi Juni 30, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mkuu huyo wa nchi pia amemwapisha Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Luteni Jenerali Salum Haji Othman.


Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao wa jeshi, Rais Samia amemshukuru na kumpongeza Jenerali Mabeyo kwa kumaliza salama kazi yake baada ya kulitumikia jeshi la wananchi kwa zaidi ya miaka 40.

“Namshukuru Mungu kwa kumjalia Jenerali Mabeyo kumaliza kazi leo akiwa smart na bado ana nguvu. Nikushukuru Jenerali Mabeyo kwa kazi nzuri uliyofanya katika utumishi wako wa zaidi ya miaka 40 jeshini.

“Umefanya kazi yako kwa uadilifu mkubwa, umetumikia cheo chako kwa jitihada kubwa na umemaliza na kukabidhi kwa wengine. Tunakushukuru sana na tunakupongeza sana kwa sababu siyo kazi rahisi,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, amemuahidi kwamba wataendelea kumteua katika majukumu mengine huku akisisitiza kwamba tayari Katibu Mkuu Kiongozi, Hussein Kattanga ameshampangia majukumu mengine.

“Unaacha ukiwa na nguvu, ukiwa bado kijana na kwa hiyo tutaendelea kukuteua, tutaendelea kukupa majukumu, uendelee kutusaidia.

“Nadhani jioni ya leo Katibu Mkuu Kiongozi atasikia kwenye bomba, tayari ameshakupangia kazi ya kufanya. Kwa hiyo tunakushukuru sana na tunakupongeza na tunakuomba bado uendelee kulitumikia taifa lako,” amesema Rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi amewapongeza pia viongozi wapya wa Jeshi la Wananchi na kuwataka kwenda kuendeleza pale alipoishia Jenerali Mabeyo.

“Niwapongeze na kuwatakia kazi njema. Mkaanze pale Jenerali Mabeyo alipoachia. Najua kwenye jeshi hakuna mtu kuingia na yake kama tulivyo kwenye serikali, ukifika mwenzio alipoachia, unaanza hapo unakwenda mbele. Maelekezo zaidi tutazungumza inbox,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk Stergomena Tax amewapongeza viongozi wapya wa JWTZ kwa dhamana waliyopewa na kuwahakikishia kwamba wizara yake itaendelea kushirikiana nao katika majukumu yao.

“Nawapongeza sana kwa uteuzi huu na ni dhamana kubwa ambayo mmepewa. Sina wasiwasi hapa kidogo nimefanya kazi na nyinyi, najua majukumu yenu mnayafahamu vizuri sana.

“Niwathibitishie kwamba tutaendelea kushirikiana na wizara itaendelea kufanya majukumu yake ya msingi kuhakikisha kwamba jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania ni imara, linaweza kutekeleza majukumu yake,” amesema Dk Tax.

Waziri Tax amemshukuru pia mkuu wa majeshi anayestaafu kwa kazi kubwa ambayo amelitumikia si jeshi tu lakini taifa kwa ujumla.

“Tunakupongeza sana na tunakutakia maisha mema baada ya kustaafu. Yapo mengi umeyafanya, yapo mengi yanaendelea, nikuhakikishie tu kwamba yale yanayoendelea tutaendelea kuyafanyia kazi sasa na timu mpya,” amesema Dk Tax.