Rais Samia aomba ushirikiano kutekeleza aliyoyahidi UNGA

Rais Samia aomba ushirikiano kutekeleza aliyoyahidi UNGA

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameomba ushirikiano kwa Watanzania ili kuyatekeleza kwa vitendo  yale aliyoahidi katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA).


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameomba ushirikiano kwa Watanzania ili kuyatekeleza kwa vitendo  yale aliyoahidi katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA).

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumamosi Septemba 25, 2021, katika hafla ya kumpokea akitokea nchini Marekani, iliyofanyika uwanja wa ndege wa Terminal 1 jijini hapa.

Amesema kuzungumza kwenye taaasisi kama ile ni jambo moja na la pili ni utekelezaji wa yale aliyoyazungumza, hivyo kuomba watanzania kushirikiana naye katika kuyatimiza

“Niliposhuka uwanjani hapa na kuona umma uliofika kunipokea nikawa kama sioni mbele na kusema sio mchezo. Ni kupitia umma huu nikawa narudi nyuma na kukumbuka yale niliyofanya kule.

“Lakini naamini umma ukishirikiana, kushikamana kwa yale niliyosema kule tutajenga nchi yetu,” amesema Rais Samia.

Kupitia hafla hiyo amewaomba Watanzania kuungana, kushirikiana, kufanya kazi kwa pamoja kujenga taifa ambalo kwa miaka 60 sasa limekuwa likijengwa kwa awamu na hatua mbalimbali na kuongeza kuwa kila awamu imekuwa ikiweka matofali katika kulijenga.

“Niwaombe kwa umoja wetu, kwa upendo wetu, tujenge kwa matoali madhubuti ili tuweze kulisimamisha vema taifa letu,” amesema.

Ametaja mambo yaliyojadiliwa katika mkutano huo likiwemo la kuathirika kwa uchumi kutokana na maambukizi ya Uviko 19, na chanjo ya maambukizi hayo na jinsi ya kushirikiana kwa nchi zilizoendelea na zinazoendelea kudhibiti na suala la utawala bora.

Kwa niaba ya Watanzania anasema aliuahidi Umoja wa mataifa kwamba Tanzani itafanyia kazi yote haya ili iende na dunia inavyokwenda.