Rais Samia apandisha thamani ya Tanzanite

Saturday July 23 2022
tanzanite pic

Mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Franone mining and Gems Ltd , Vitus Ndakize (kulia) akizungumza na warembo wanaowania taji la Miss Jungle International waliotembelea machimbo ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo

By Joseph Lyimo

Mirerani. Bei ya madini ya Tanzanite na uhitaji wa madini hayo umeongezeka mara dufu baada ya filamu ya Royal Tour kumuonyesha Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye machimbo ya madini hayo.

Katika sehemu ya filamu hiyo, inamuonesha mkuu huyo wa nchi akiwe katika machimboi hayo yaliyopo mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.

Hayo yalibainishwa juzi Alhamisi Julai 21, 2022 na mmoja kati ya wakurugenzi wa kampuni ya Franone mining and Gems Ltd, Vitus Ndakize wakati warembo nane watakaoshiriki kinyang’anyiro cha Miss Junge International walipotembelea mgodi huo.

“Bei ya gramu moja ya madini ya Tanzanite inategemea na ubora na rangi yake ila awali gramu moja ilikuwa inauzwa Sh400,000 ila baada ya Rais Samia kuonekana kwenye Royal Tour gramu moja inauzwa Sh600,000,” alisema Ndakize.


Alisema mara baada ya kipande cha filamu hiyo ya Royal Tour kuonekana na Rais Samia akiwa katika mgodi huo wa Tanzanite, bei ya madini imepanda na uhitaji wake umeongezeka zaidi.

Advertisement

“Ni fursa pekee sisi wazalishaji kufanya kazi, kwani uhitaji wa madini ni mkubwa na bei imepanda na tumefaidika kupitia Rais Samia kuyatangaza madini yetu kwenye filamu ya Royal Tour,” alisema Ndakize.

Sekta hiyo ya madini imekuwa ikipiga hatua ambapo Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko akiwasilisha bajeti yake bungeni yam waka 2022/23 alisema, biashara ya madini nchini imeendelea kuimarika.

Alisema katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Machi 2022 jumla ya kilogramu 39,682.94 za dhahabu, kilogramu 7,102.96 za fedha, karati 155,117.10 za almasi, kilogramu 15,377.44 za Tanzanite ghafi.

Alisema kilogramu 130,582.28 za Tanzanite za ubora wa chini (beads), karati 81,305.42 za tanzanite iliyokatwa na kusanifiwa, 25 tani 19,355.13 za madini ya shaba na tani 322.49 za madini ya bati zilizalishwa.

Aidha, Dk Biteko alisema alisema marekebisho ya sheria na kanuni yanaelekeza biashara ya madini ya Tanzanite pamoja na shughuli zote za ukataji, ung’arishaji au shughuli za uongezaji thamani madini kufanyika ndani ya Eneo Tengefu la Mirerani au eneo lolote la Mirerani litakaloidhinishwa kwa maandishi.

Alisema Kanuni hizo zilizoanza kutumika tarehe 9 Julai, 2021 zilitangazwa katika Tangazo la Serikali Na. 592 la tarehe 9 Julai, 2021.

Waziri huyo alisema kukamilika kwa ujenzi na usimikaji wa miundombinu ikiwemo taa, kangavuke, kamera za ulinzi na barabara inayozunguka ukuta kwa ndani katika Eneo Tengefu la Mirerani, udhibiti wa utoroshaji wa madini ya Tanzanite umeimarika.

Alisema hatua zilizochukuliwa na Serikali zimeboresha upatikanaji wa tozo stahiki zinazotokana na biashara ya madini hayo.

“Kabla ya ujenzi na usimikaji wa miundombinu, uzalishaji ulikuwa kilogramu 1,964.75 kwa mwaka 2018/2019 ikilinganishwa na kilogramu 3,198.65 za tanzanite zilizozalishwa kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Machi 2022,” alisema Dk Biteko

Katika ziara hiyo ya warembo, Mratibu wa Bega kwa bega na Mama Foundation wanaoandaa mashindano ya Miss Jungle International, Martin Rajab alisema lengo la ziara hiyo ni kutangaza zaidi madini hayo na mashindano hayo yatashirikisha warembo 50.


Miss Jungle International Tanzania, Dorine Gibson alisema amefurahia kufika kwenye eneo la machimbo ya madini ya Tanzanite na kuona sehemu pekee yanapopatikana duniani.

Naye Miss Jungle International Zanzibar, Zuhura Makame alisema watayatangaza madini ya Tanzanite ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Royal Tour.

Kwa upande wake, Miss Jungle International Kenya, Wendy Wamanga alihoji ni sababu gani madini ya Tanzanite yanapatikana Tanzania pekee na hayapatikani sehemu nyingine yeyote duniani?

Mnyange wa Miss Jungle International Czchek, Sarah Horakova alisema amefurahia kufika kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite kwani amekuwa mwanamke wa kwanza kutoka kwenye nchi yake kuingia mgodini.

Kaimu ofisa madini mkazi wa Mirerani, mhandisi Castro Maduwa aliwakaribisha warembo hao na kuwajulisha kuwa wao wanasimamia mchakato mzima wa uchimbaji, tathimini na uuzaji wa madini hayo.

Katibu wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (Marema) Tariq Kibwe alisema fursa ya warembo hao kutembelea machimbo ya Tanzanite ni kuzidi kuyatangaza zaidi kimataifa.

Advertisement