Rais Samia ataja sababu kutoelewana wabunge, wakurugenzi

Rais Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono wananchi waliojipanga kando kando ya barabara ya Tabora - Mpanda katika eneo la Sikonge mara baada ya kuifungua barabara hiyo.Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amesema baadhi ya viongozi katika halmashauri nchini wanashindwa kuelewana kutokana na kutofuatwa kanuni za fedha.
  • Mkuu huyo wa nchi amewahakikishia wananchi kuwa hawapaswi kutozwa wanaposafirisha mazao yao yaliyo chini ya tani moja.

Tabora. Rais Samia Suluhu Hassan amesema baadhi ya viongozi katika halmashauri nchini wanashindwa kuelewana kutokana na kutofuatwa kanuni za fedha.

Rais Samia amebainisha hayo leo Alhamisi Mei 19, 2022 wakati akizungumza na wakazi wa Mkoa wa Tabora katika siku yake ya mwisho ya ziara ya siku tatu mkoani humo.

Amesema kuwa kukwepwa kwa kanuni za fedha ndio kumesababisha kutokueleaa kwa baadhi ya viongozi wakiwamo wabunge na wakurugenzi wa halmashauri  huku akisema dawa yake ni kufuatwa kwa kanuni hizo za fedha na migongano hiyo haitakiwepo.

Amesema ili kuepuka hali hiyo mabaraza ya madiwani yanapaswa kuchukua nafasi yake kwa kutoa maamuzi ya mambo kwenye halmashauri zao.

Rais Samia alikuwa akijibu malalamiko ya Mbunge wa Manonga, Seif Gulamali aliyemlalamikia mkurugenzi mtendaji wa halmashauri yake kuwa amekataa kutoa fedha za halmashauri Sh100 milioni kuunga mkono fedha alizotafuta kwa wafadhili Sh500 milioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Amesema kuwa alipata fedha Sh500 milioni kutoka kwa wafdhili kwaajili ya miradi ya maendeleo lakini ilitakiwa Sh100 milioni zitoke halashauri kuunga mkono fedha hizo alizozitafuta kwa wafadhili ambapo amedai kuwa mkurugenzi alikataa kutoa.

Amesema kuwa pamoja na kufikisha suala hilo kwa mkuu wa mkoa, amesema limeshindwa kushughulikiwa.

"Mheshimiwa Rais mimi kazi yangu kutafuta fedha kwa ajili ya maendeleo ya Jimbo lakini mkurugenzi amegoma kutoa fedha " amesema.

Mbunge huyo ameeleza kuwa hata alipotaka fedha hizo kutoka mfuko wa maendeleo ya Jimbo, bado mkurugenzi alikataa.

Rais Samia amesema kama kanuni za matumizi ya fedha zikifuatwa kunakuwa hakuna tatizo.

"Kama kanuni za fedha zinafuatwa hakuna kusikiliza ugomvi wa matumizi ya fedha" amesema Rais Samia ambaye yuko mkoani Tabora kweneye ziara ya siku tatu.

Ametaka mabaraza ya madiwani nchini kujadili matumizi ya fedha na kama wakiyapitisha wanakuwa na wajibu wa kuyasimamia maamuzi yao.


Awajibu wabunge

Mkuu huyo wa nchi amewahakikishia wananchi kuwa hawapaswi kutozwa wanaposafirisha mazao yao yaliyo chini ya tani moja.

Amesema agizo hilo ambalo lilitolewa na mtangulizi wake kuwa bado hajalifutwa huku akiwataka wenye mazao yasiyozidi tani moja wanaweza kuendelea kuyasafirisha bila kutozwa tozo.

Rais Samia ambaye alikuwa anajibu ombi la Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka aliyedai kuwa wananchi wanasumbuliwa kwa kutozwa tozo ya mazao hadi debe moja, amewataka wananchi kutokuwa na wasiwasi kwani agizo linasimama lilivyo na kuongeza kuwa huenda hata mgambo huwa hawapeleki fedha sehemu husika wakizichukua.

Kuhusu wajawazito kulipishwa wakati wa kujifungua, amesema wataisimamia MSD inunue vifaa vyote vya kujifungulia ingawa pia ameeleza kwamba suala hilo litatokewa tamko rasmi baadaye.

Rais Samia alikuwa akijibu madai ya mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Tabora, Munde Tambwe aliyedai kuwa wajawazito wamekuwa wakitozwa fedha wanapoenda kujifungua japokuwa wamekuwa wakiambiwa kuwa kujifungua ni bure.

Akijibu ombi la mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka aliyelalamika wananchi kisumbuliwa na hata kutolewa kwenye maeneo yao pasipo kulipwa fidia ambapo imesababisha mgogoro kwa wananchi waliokaribu na eneo la Jeshi, Rais Samia amesema ameichukua changamoto hiyo na anaenda kuifanyia kazi.


Ataka miradi itumike kuwanufaisha wananchi kiuchumi


Rais Samia ambaye leo anahitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani hapo, amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kuwasisitiza wananchi kuchangamkia fursa za ajira katika miradi ya maendeleo.

Amesema wakati miradi inajengwa kuna fursa za moja kwa moja na pia kwa wafanyabiashara ya kuuza chakula na bidhaa zingine.

"Changamkieni fursa ya uwepo wa mradi ya maendeleo vinginevyo watachukua bidhaa sehemu nyingine" amesema.

Amesema wananchi watumie kunufaika kwa kuajiriwa au kujiajiri wenyewe.

Rais Samia amewatia moyo mawaziri wake kuwa wachape kazi na wasisumbuliwe na maneno kwani hata yeye anapata maneno mengi.

“Mawaziri hawa ni vijana naomba niwatie moyo chapeni kazi" amesema baada ya kiwasimamisha mawaziri Bashe, Aweso, Bashungwa na Makamba.

Rais Samia anamaliza rasmi ziara yake ya siku tatu mkoani Tabora leo ambapo alitembelea Wilaya za Uyui, Sikonge na Tabora na kuzindua miradi ya barabara inayounganisha mkoa wa Tabora na mikoa ya Singida na Katavi.