Rais Samia atengua uteuzi vigogo watatu

Monday May 03 2021
samia pc
By Fortune Francis

Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa viongozi watatu akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (Tasac), Profesa Tadeo Andrew Satta.

Sambamba na hatua hiyo, pia Rais Samia pia ametengua uteuzi wa wajumbe sita wa bodi ya Tasac.

Aprili 6, mwaka huu wakati Rais Samia akiwaapisha viongozi mbalimbali alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Tasac Kaimu Abdi Mkeyenge kwenda kurekebisha upungufu uliomo ndani ya Tasac.
Rais Samia alitaja miongoni mwa upungufu huo kuwa pamoja na kutumia zaidi ya Sh600 milioni kwaajili ya kufanya vikao 23 vya bodi.

Taarifa iliyotolewa leo Mei 03, 2021 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga imeeleza, mbali na Profesa Satta, Rais Samia pia ametengua uteuzi wa Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Hassan Mwang’ombe.

Wengine ambao uteuzi wao umetenguliwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania Dk Harun Kondo.

“Sambamba na hatua hiyo, Rais Samia pia amevunja Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uteuzi wa viongozi watakaoshika nyadhifa hizo utafanywa baadaye.

Advertisement
Advertisement