Rais Samia atoa maagizo 8 kwa wateule wake

Rais Samia akizungumza leo Machi 4, 2023 katika mkutano wa faragha kwa mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali jijini Arusha.

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka wateule wake kuzingatia maeneo manane ya msingi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ikiwa pamoja na kuwa viongozi bora, huku akiwataka kuanza upya, kwani yaliyopita si ndwele.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka wateule wake kuzingatia maeneo manane ya msingi, ikiwamo kujiamini katika utekelezaji wa majukumu yao.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Machi 4, 2023 katika mkutano wa faragha kwa mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali jijini Arusha.

“Lakini unapokuwa unajiamini hakikisha pia unakuwa tayari kuutetea uamuzi uliofanya, lingine ni kuendeleza rasilimali watu, hili ni eneo muhimu sana, usipopanga vizuri kwamba akitoka huyo miaka 60 huyu yupo anachukua nafasi kwa uhakika.

“Usipowapanga vizuri, unapanga future ambayo haina future. Kila mmoja akijiamini anaweza kuchukua kazi ya bosi wake na kwenda nayo, basi unapanga future yenye future.

“Tafuta watu wenye nia ya kufanya mambo yafanikiwe, usichukue watu ambao anakuja kuendeleza ile routine (ratiba) iliyozoeleka, leta watu wenye mawazo mapya, leta mtu atakayekusaidia kufikiri mambo mambo mapya ya taasisi yako,” amesema.   

Katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo wa mafunzo mahususi, Rais Samia ametaja eneo la tatu kuwa ni umuhimu wa kufanya kazi na sekta binafsi ili kupata mitaji mikubwa itakayosaidia katika utekelezaji wa miradi yenye kuongeza ajira, vyanzo vipya vya mapato na uzalishaji.

Nne, ni kuweka mbele ya masilahi ya Taifa katika jambo wanalohusika kwenye utekelezaji, kuongeza ubunifu katika utendaji wao, kuachana na utumwa wa sheria zinazokwamisha utekelezaji wa mipango iliyopo na kujenga utamaduni wa mawasiliano kwa njia ya mifumo ya serikalini.

Saba ni  kuzingatia mafunzo huku akiagiza Taasisi ya Uongozi kurejesha utamaduni wa mafunzo kwa watendaji hao, utekelezaji wa mipango ya Serikali na utoaji wa taarifa hizo kwa wakati pamoja na kutathmini kiapo chao cha kulinda, kuhifadhi na kuitetea Katiba ya Jamuhuri ya Muungano.

Kuhusu kujitambua kama viongozi wa Jamhuri ya Muungano, amesema;

“Tunasema mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na sisi ni Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.”