Rais Samia awafunda mawaziri, naibu mawaziri

Rais Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan leo Alhamisi Januari 13, 2022 amezungumza na mawaziri na naibu mawaziri jijini Dodoma.

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan amezungumza na mawaziri na naibu mawaziri huku akibainisha mambo mawili ambayo amesema ni maradhi yanayozitesa wizara mbalimbali.

Rais Samia amezungumza na mawaziri na naibu mawaziri hao leo Alhamisi Januari 13, 2022 jijini Dodoma.

Akieleza mambo ambayo amewataka mawaziri na naibu mawaziri kuyazingatia kwenye wizara zao, ametaja mambo mawili ambayo amesema ni kama maradhi kati ya watendaji wa wizara mbalimbali.

đź”´#LIVE: Rais Samia akizungumza na mawaziri, naibu mawaziri

Jambo la kwanza mabalo Mkuu huyo wa nchi amelitaja kuwa changamoto kwenye wizara mbalimbali ni kushindwa kutunza siri za Serikali na kuachia nyaraka kupenya kwenye mitandao ya kijamii.

Rais Samia ambaye alikuwa anazungumza huku mawaziri na naibu mawaziri wakiwa wanaandika amesema “Suala la pili ni masuala ya kutunza siri zetu za Serikali, hii imekuwa kama maradhi, documents (nyaraka) za Serikali tunazikuta kwenye mitandao, watu wanabishana huko watu wanaenda kuchomoa documents, inapigwa picha inawekwa kwenye mtandao, sasa hili halipendezi na hakuna Serikali inayoendeshwa namna hiyo” amesema nakuongeza 

“Serikali inatoka kwenye ofisi zetu inaenda kwenye mitandao, hatuendi hivyo, naomba mkalisimamie hilo, kudhibiti siri za Serikali”

Akitaja jambo la pili ambalo ni miongoni mwa aliyosema kuwa ni maradhi yanayozisumbua wizara, Rais Samia amesema

“Suala lingine ni kutoelewana baina yenu, sijui mna maradhi gani ndugu zangu, waziri na naibu waziri hawaelewani, waziri na katibu mkuu hawaelewani, hili mimi silielewi kwa sababu kila mtu yuko pale ameonekana anaaminika na anaweza kufanya hiyo kazi”

Amesema kuwa baadhi ya migogoro kati ya viongozi hao ni kutokana na kugombania maslahi binafsi na si kwa ajili ya maslahi ya wananchi

“Lakini kinachotokea huko ni migongano, mnagombania safari, safari ilikuwa yangu anakwenda yeye tu, mnagombaniana sijui kitu gani wakati sekta ni kubwa” amesema

“Wakati mwingine mnachogombania sio haki zenu, ni kwa haki za wananchi mnazozi-grab, lakini huko kwa sababu mgawo hauendi sawa mnagongana” amesema