Rais Samia awalilia waliofariki ajalini Shinyanga

Muktasari:

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemtumia salamu za rambirambi, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema kutokana na ajali iliyotokea mkoani mwake na kusababisha vifo na majeruhi, usiku wa kumakia leo Jumanne.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametuma salamau za rambirambi kufuatia vifo vilivyotokea katika ajali Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga.

 Ajali hiyo imehusisha gari ndogo aina ya IST, Hiace na Lori, usiku wa kuamkia leo Jumanne, Agosti 9, 2022, eneo la Mwakata.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema, Rais Samia ametuma salamu hizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema kufuatia vifo vya watu 16 na majeruhi 11.

Taarifa hiyo imemnukuu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Leonard Nyandahu akisema waliopoteza maisha ni 16, kati yao wanawake ni wawili na wanaume 14 huku majeruhi 11, wanawake wanne wanaume saba waliopelekwa hospitali ya Kahama.

Katika ajali hiyo, watu waliokuwepo kwenye dogo aina ya IST walifariki papo hapo na dereva wa trekta kukimbia.

Rais Samia amevitaka vyombo vinavyosimamia usalama barabarani kuongeza juhudi ya kudhibiti ajali huku akiwapa pole wafiwa na anaungana na familia hizo katika kipindi kigumu cha majonzi.

“Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi. Amani,” imesema taarifa hiyo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Dk Deogratius Nyaga amesema, wamepokea miili 20 na majeruhi 15 ambao watatu kati yao hali zao siyo nzuri.