Rais Samia azindua barabara ya Njombe-Makete

Muonekano wa Barabara ya Njombe-Makete kilomite 107.4 ambayo imefunguliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla iliyofanyika Makete Mkoani Njombe leo Jumanne Agosti 9, 2022.


Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan amezindua ujenzi wa barabara ya Njombe-Makete akisema itafungua fursa za uchumi kwa wanananchi wa mkoa huo.  

Njombe. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Njombe-Makete kutafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Kauli hiyo ameitoa leo Jumanne Agosti 9, 2022 wakati wa uzinduzi wa barabara hiyo akisema barabara hiyo ina umuhimu, kwani pia itaunganisha wilaya hiyo na mikoa na nchi zinazopakana na Tanzania.

Mbali na kufungua masoko, Rais Samia amesema pia barabara hiyo itafungua utalii hasa kutokana na hifadhi zilizopo wilayani humo.

"Lakini niwaambie jambo moja barabara hii ya Makete tumeisubiri kwa muda mrefu sana na fedha iliyotumika kujenga barabara hii ni zaidi ya Sh100 bilioni kwa kilomita zote 107.

“Ombi langu kwa Wanamakete ni kuilinda barabara hii," amesema Samia.

Amewaonya watu wenye tabia ya kuchimba mchanga na madini chini au kando ya barabara, kuacha mara moja tabia hiyo.

Awali akizungumza, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali inafahamu kuwa wananchi wa wilaya hiyo wanapata mahitaji yao kwa kiasi kikubwa kutoka Mkoa wa Mbeya, hivyo ilikuwa ni lazima barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 203.6 kujengwa.

Amesema mkandarasi wa kujenga barabara hiyo amepatikana na anatarajia kuanza kazi mwezi ujao kwa kujenga kipande cha kutoka Kitulo mpaka Inyuho chenye urefu wa kilomita 36.3.

"Mheshimiwa Rais tumechagua kipande hiki kwa sababu eneo hilo ni korofi sana na mvua ikinyesha halipitiki," amesema Mbarawa.

Amesema vipande vinavyofuata mkandarasi atawekwa kuanzia Makete ili wakutane na yule anayeanzia Kitulo ili barabara hiyo iwe kuwa na lami asilimia mia moja.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Rogatus Mativila amesema barabara hiyo inaunganisha makao makuu ya mkoa wa Njombe na wilaya ya Makete ni muhimu kwa wananahci wa mkoa huo.