Rais Samia: Hatutarudi nyuma

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde pamoja na viongozi mbalimbali wastaafu wa Afrika wakiwa kwenye Mkutano wa Mtandao wa Viongozi Wanawake wa Afrika uliofanyika Zanzibar Desemba 03, 2022.

Muktasari:

Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akisema Tanzania inazidi kupiga hatua kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi wanawake, viongozi wakuu wa nchi za Afrika wamesema bado Afrika inapaswa kuongeza nguvu kuwainua wanawake kiuchumi na kuwaondolea vikwazo.


Unguja. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akisema Tanzania inazidi kupiga hatua kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi wanawake, viongozi wakuu wa nchi za Afrika wamesema bado Afrika inapaswa kuongeza nguvu kuwainua wanawake kiuchumi na kuwaondolea vikwazo.

Haya yamesemwa juzi, katika mkutano wa nne wa mtandao wa viongozi wanawake Bara la Afrika uliofanyika mjini hapa na kuwashirikisha wanawake viongozi mbalimbali, wakiwamo marais wa sasa na wastaafu wa Afrika.

Lengo la mkutano huo wa siku nne kuanzia Desemba 2 hadi 4, ni kujadili changamoto na fursa kwa wanawake katika kuleta usawa.

Akizungumza katika mkutano huo ambapo alikuwa mgeni rasmi, Rais Samia alisema Serikali anayoiongoza inajitahidi kuwaweka wanawake katika ngazi mbalimbali za uamuzi, huku akisema kuwa wameonyesha utendaji kazi uliotukuka.

Akithibitisha hilo, alisema idadi ya wanawake kwenye ngazi za uamuzi na uongozi inaongezeka ikilinganishwa na taifa hilo lilipotoka, akitolea mfano wa wabunge wanawake kuongezeka kutoka asilimia 21.5 mwaka 2005 hadi asilimia 37 mwaka huu.

Kutoka asilimia tatu ya mawaziri hadi kufikia asilimia 21, majaji asilimia 47, mahakimu wa mikoa na wilaya kutoka asilimia 25 hadi asilimia 38, wakuu wa mikoa kutoka asilimia 10 hadi 23 na wakuu wa wilaya kutoka asilimia 19 hadi asilimia 25.

“Takwimu hizi zinaonyesha haturudi nyuma tunasonga mbele, hawa wanawake wamepewa nafasi na wameonyesha uthibitisho kwamba wanaweza na wanachapa kazi, lazima tutumie fursa hii kufungua fursa kwa ajili ya wanawake,” alisema Rais Samia.

Alishauri mataifa ya Afrika kuwekeza zaidi kwenye takwimu za kijinsia ambazo zitawaonyesha uhalisia na kupata mwelekeo mpya wa wanapotaka kwenda ambapo Tanzania imeanza kuonesha hilo na kutekeleza kizazi cha usawa.

Alisema pia Tanzania inaweka vipaumbele vyake katika kuhakikisha wanawake wanamiliki uchumi kwa kuwawezesha kiujasiriamali kwa kuwapa mikopo, kuongeza bajeti na kupitia malengo hayo nchi, imeweza kuimarisha mambo hayo.

Alisema yameanzishwa majukwaa ya wanawake zaidi 3,000 na mkakati uliopo ni kuanzisha majukwaa hayo katika ngazi ya vijijini na kuhakikisha wanaweza kuingia katika masoko huru ya kikanda.

Rais Samia, aliyeingia madarakani Machi 19 mwaka jana kufuatilia kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli alisema wanawake sio tena watu wa kukaa nyumbani kama ambavyo imezoeleka, bali wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wao.

Hata hivyo, Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akitoa takwimu hizo za kuongezeka kwa wanawake kwenye nafasi mbalimbali, hali bado iko nyuma ndani ya chama hicho.

Itakumbukwa mwaka 1995 katika mkutano wa nne wa kimataifa wa wanawake uliofanyika Beijing, China walikubaliana kwa pamoja kuwa ni lazima kufikia usawa wa kijinsia wa 50 kwa 50 ifikapo mwaka 2030.

Matokeo ya chaguzi za CCM kuanzia Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Jumuiya za Wazazi, Wenyeviti wa Mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar yanaonyesha hali bado ni ngumu.

Katika nafasi 95 zilizowaniwa kwenye chaguzi hizo za ngazi ya mikoa, wanawake 12 pekee walishinda, takwimu hizo ni sawa na asilimia 12.6 na wanaume walioshinda walikuwa 83, sawa na asilimia 87.36.

Chaguzi za uenyeviti wa mikoa na Jumuiya ya Wazazi wa CCM hali imeonekana kuwa mbaya ambapo ni wanawake watatu tu kwa kila nafasi hizo mbili walishinda, sawa na asilimia 9.3.

Kwa upande wa UVCCM, kati ya wenyeviti 31 waliochaguliwa nchini, wanawake walikuwa sita, sawa na asilimia 19.35, huku wanaume wakiwa 25, sawa na asilimia 80.65.


Alichosema Rais Zewde

Katika mkutano huo wa viongozi wanawake, Rais wa Ethiopia, Sahlework Zewde alisema Tanzania ni sehemu salama ya kufanya mkutano huo kutokana na historia yake na hatua mbalimbali ambazo imefikia katika ukombozi wa wanawake.

“Tunajua Tanzania imekuwa mstari wa mbele kuleta uhuru barani Afrika, imeshiriki kwa nchi nyingi.

Mbali na hilo, alisema ipo michakato mingi ya kuleta suluhishi na amani imefanyika hapa nchini.

Alisema kuna mabadiliko mengi ya kimfumo duniani kwa sasa, jambo linaloonyesha wazi kwamba hakukuwa na usawa wa kijinsia, hivyo ipo haja ya kuondoa vikwazo vinavyowanyima wanawake kufikia ndoto zao.

“Tunapaswa kuangalia vikwazo hivi na kujadili mitazamo hasi iliyopo juu ya wanawake ili kuwafanya wawe salama na kuwaweka katika shughuli za uchumi.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa vijana, Chido Mpemba alisema zinapoandaliwa programu zinatakiwa kuwapo rasilimali za kutosha kuwasaidia wanawake kushirikishwa katika maamuzi katika ngazi za kutengeneza sera, na kuwapa wanawake uongozi.

Awali, Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Afrika, Amina Mohamed alisema wanatengeneza mfumo mpya ambapo bara la Afrika litahitaji mkakati mpya wa kukuza ujuzi kwa vijana.