Rais Samia: Tutaendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameendelea na ziara ya kikazi Mkoa wa Njombe kwa kukagua na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo.

Njombe. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kusogeza huduma za afya kwa wananchi kama ambavyo ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi imeelekeza.

 Amesema hayo leo Jumanne Agosti 9, 2022, wakati akikagua jengo la huduma za afya ya mama na mtoto lililopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.

Rais Samia amesema ilani ya CCM imeelekeza kusogeza huduma za afya kwa wananchi na jambo hilo lingefanyika muda mrefu nyuma lakini kwakuwa kazi ya Serikali ni hatua kwa hatua.

"Nataka niwahakikishie yale yote tuliyoagizwa na Chama Cha Mapinduzi sisi Serikali tunakwenda kuyatekeleza," amesema Rais Samia.

Amesema kwa kipindi hiki yote hayo yameweza kufanyika ya kusogeza karibu huduma za afya kwa wananchi na hiyo imefanyika kwa nchi nzima.

Amesema Serikali imekuwa ikijitahidi kufanya vema katika kusogeza huduma mbalimbali kwa wananchi na kama kuna maeneo kuna changamoto kote kuna hatua za kuchukua.

Awali, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuna kazi kubwa inafanyika mkoa wa Njombe kujenga vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya na hospitali ya rufaa ya mkoa wa Njombe.

Amesema jengo la huduma za afya ya mama na mtoto limekamilika likiwa na wodi, jengo la maabara, ICU na EMD.

Amewataka wananchi wa mkoa wa Njombe kuendelea kumuunga mkono Rais Samia kwa kuwa anaendelea kufanya kazi ya kuleta maendeleo kwa wananchi.

"Tulianza 2016 na jengo moja lakini ndani ya kipindi kifupi cha Rais Samia Suluhu Hassan ameshasimamisha majengo matano katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Njombe," amesema Ummy.