Ratco: WanaCCM wasiwadharau wapinzani

Muktasari:

  • Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa mkoa wa Tanga (MNEC), Mohamed Salim Ratco amewataka wanachama wa chama hicho kuacha tabia ya kudharau vyama vya upinzani na badala yake wajiimarishe.

Handeni. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa mkoa wa Tanga (MNEC), Mohamed Salim Ratco amewataka wanachama wa chama hicho kuacha tabia ya kudharau vyama vya upinzani na badala yake wajiimarishe.

Ratco amesema hayo akiwa kwenye ziara yake ya ufuatiliaji utekelezaji wa Ilani ya chama, utekelezaji wa misingi ,miongozo na kanuni za CCM pamoja kukagua miradi ya maendeleo ya chama hicho wilayani Handeni

Amesema licha ya kwamba CCM inafanya vizuri kwenye chaguzi zake lakini isiwe ni kigezo cha wanachama wake kudharau vyama vya upinzani vilivyopo nchini.

“Upinzani upo tusidharau maana hatuwezi kufahamu na wao wanawaza nini kuhusu sisi. Licha ya kwamba kuna upinzani wa ndani kwa ndani, huo tunaumudu kuufanyia kazi wenyewe,” amesema Ratco.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa CCM wilaya ya Handeni, Athumani Malunda amesema katika uchaguzi uliopita wapo watu walikuwa wapinzani ndani ya chama, hivyo ametaka kwenye uchaguzi ujao wa chama, wachukuliwe hatua.

Ameongeza kuwa kama alikuwepo mtu wa ndani wa CCM lakini anasaidia upinzani, hafai na anatakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu kupitia chama.

Kwa upande wake, kaimu katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT), Aisha Mpuya amewataka wanaCCM kuzingatia maadili ya chama hicho ikiwemo kutochafuana kutokana na mambo ya kugombea uongozi.

Katika ziara hiyo, Ratco ametoa bati 50 kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa nyumba ya katibu wa CCM Handeni, pia amechangia laki sita kwa ajili ya kununua simu ya kusajili wanachama kwa njia ya Tehama.