RC Chalamila asimamia ubomoaji nyumba ya mwananchi aliyegoma kuhama

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila.

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesimamia shughuli ya kubomoa nyumba ya Aton Lyuba (75) anayedaiwa  kukaidi agizo la kuibomoa mwenyewe kupisha mradi wa barabara akitaka alipwe fidia.

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesimamia shughuli ya kubomoa nyumba ya Aton Lyuba (75) anayedaiwa  kukaidi agizo la kuibomoa mwenyewe kupisha mradi wa barabara akitaka alipwe fidia.

Chalamila ametekeleza jambo hilo leo Jumanne Desemba 15, 2020 baada ya  kuelezwa kuwa mwananchi huyo ndio chanzo cha mradi huo wa barabara yenye urefu wa kilomita 16.7  kutokamilika.

"Nimefikia hatua hii leo kwani tumekaa naye zaidi ya mara nane lakini hataki kubomoa anahitaji fidia wakati eneo hilo kwenye ramani ni la miradi ya maendeleo ya wananchi.”

“Tumembembeleza sana kubomoa na ukiangalia miradi mingi kwa sasa makandarasi wanakimbizana na mvua kuhakikisha miradi inakwisha kwa wakati na si kukwamishwa na watu wachache,” amesema Chalamila.

Amebainisha kuwa umefika wakati wananchi kuunga mkono jitihada za Serikali kwani miundombinu hiyo ni faida yao katika kukuza uchumi.

Mhandisi wa mradi wa wakala wa  barabara za mijini na vijijini (Tarura), Imelda Ngailo amesema ulianza Aprili, 2020 na umekwama kutokana na mkazi huyo kugoma kubomoa nyumba yake akihitaji fidia.

"Ndio maana mnaona maeneo mengine mradi umeenda vizuri lakini kufika hapa tumekwama ingawa tumemsihi mara kadhaa abomoe lakini amekaidi agizo letu na serikali," amesema.

Kwa upande wake Lyuba alikana kufuatwa kutakiwa kubomoa nyumba yake, akisisitiza kuwa hakugoma kupisha mradi bali aliomba kulipwa fidia.