RC Homera aagiza Brela kudhibiti fedha haramu

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera akifungua kikao cha wadau, Makampuni binafsi kilichoitishwa na  Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela). Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Ametoa agizo hilo kwenye kikao cha wadau kilichoitishwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kilicholenga kuhamasisha kuhusu kanuni za wamiliki manufaa.

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ameagiza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kuharakisha kutumia mabadiliko muswada sheria fedha ya mwaka 2020 ya urasimishaji wa makampuni ili kudhibiti uingizwaji wa fedha haramu na ufadhiri wa vitendo vya ugaidi.

Homera amesema leo Jumatano, Machi 29, 2023 wakati akifungua kikao cha wadau kutoka sekta mbalimbali hususan makampuni, wanasheria, wahadhiri, wafanyabishara na taasisi za kifedha kilichofanyika jijini hapa.

“Bunge kupitia muswada wa Sheria ya Fedha mwaka 2020 ilipitisha mabadiliko ya sheria za makampuni kwa lengo la udhibiti wa upatikani wa fedha haramu na  vitendo vya ugaidi kwa kampuni ikiwepo  wamiliki kurasimisha kwenye mifumo kwa  kutoa taarifa husika brela,” amesema.

Amesema mfumo wa umiliki manufaa ni mpya wenye  lengo ni kudhibiti uwepo wa makampuni yanayotumika vibaya  kuingiziwa fedha haramu  hususan kuchochea vitendo vya kigaidi .

“Baada ya Bunge kupitia muswada  wa sheria limefanya jambo jema kwa Brela kuanza utekelezaji wa upokeaji wa taarifa za urasimishaji wa makampuni ikiwa ni kutekeleza agizo la Serikali ,sambamba na utoaji wa elimu,” amesema.

Isdor Mkindi ambaye ni Mwakilishi wa Ofisa Mtendaji Mkuu Brela, Godfrey Nyaisa, amesema kuwa wamiliki wa kampuni wanatakiwa kujisajili na kuyarasimisha kupitia mifumo ya kimtandao kabla ya sheria kuanza kuchukua mkondo wake.

Amesema kuwa wamekuja mkoani Mbeya kutokana na mwamko mkubwa wa kampuni kurasimisha biashara na kuonya watakaokwepa kujisajili watachukuliwa hatua za kisheria ikiwepo kutizwa faini kulingana na muda wa ucheleweshwaji wa kuwasilisha taarifa.

Naye Mkuu wa Kitengo cha uhusiano Brela makao makuu, Roida Andusamile amesema kuwa mwitikio wa kampuni ni  mkubwa na lengo kubwa ni kuendelea kuwapatia elimu ya umuhimu wa kusajili na kurasimisha kupitia mifumo rasmi ya kiserikali katika uendeshaji .

Mdau kutoka Taasisi ya kufedha, Groly Nnko amesema  utaratibu huu utawasaidia kubaini uingizwaji holela fedha haramu jambo ambalo litawezesha kubaini kampuni zinayofanya vitendo hivyo.

“Tulishukuru Bunge na pia Serikali kwa kuliona hilo kwani litasaidia sana taasisi zetu kubaini kwani usajili wa kampuni pia utakuwa mwiba wa kubaini yasiyoingia kwenye mfumo wa Brela,”amesema.