RC Katavi agoma kuongeza muda ujenzi bandari Karema

Wednesday October 13 2021
rc katavipic
By Mary Clemence

Katavi. Mkuu wa mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amesema hatakubali maombi ya kampuni ya Xiamen On Going Construction Group ya kuongeza muda wa ujenzi wa Bandari ya Karema katika ziwa Tanganyika.

Mrindoko amebainisha hayo Jumatatu Oktoba 11, 2021 alipofanya ziara ya kukagua mradi huo na kubaini kuwa mkandarasi ameshindwa kwenda na muda uliowekwa awali.

Amesema mradi huo umefikia asilimia 60 huku akibainisha muda uliotolewa awali unatosha kukamilisha kazi hiyo.

"Asilimia 40 iliyobaki ni kubwa sana kwa hiyo, ongezeni kasi ya ujenzi ili kufikia Machi 6, 2022 uwe umekamilika kwa asilimia 100. Hatupendi kusikia tena mnaomba extension of time (nyongeza ya muda) kwasababu hakuna kikwazo chochote.

"Upande wa Serikai hakuna tatizo malipo yanafanyika mmeeleza hapa, ukamilishwe na ukabidhiwe kwa muda muafaka," alisema Mrindoko.

Katika hatua nyingine amewataka wasimamizi wa mradi huo kutoa taarifa mapema pindi wanapobaini kuwepo vitendo vya uhalifu eneo la mradi ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Advertisement

"Wale waliojihusisha na wizi wa vifaa vya mradi, watakamatwa. Vfaa vyote vinatakiwa kutumika, vikisalia vitarudishwa serikalini kufanya kazi nyingine. Hatutafumbua macho mambo ya hovyo, mjirekebishe," amesema.

Awali Mwakilishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) wanaosimamia mradi huo, Mhandisi Joseph Urasa amesema mradi huo kwasasa umefikia asilimia 60 upo nyuma kwa asilimia mbili,  akiongeza kuwa changamoto kubwa zinazoukabili mradi huo ni ucheleweshwaji wa ununuzi ya vifaa vya ujenzi ikiwamo saruji.

"Hili la ununuzi vifaa tumemshauri mkandarasi kuongeza kasi ya kifanya manunuzi mapema na kusafirisha kutoka kiwandani hadi eneo la mradi," amesema Urasa kaongeza.

Ametaja pia changamoto za wizi wa mafuta na vifaa vya ujenzi akisema wameshafikisha taarifa kwa vyombo vya usalama.

Advertisement