Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RC Kilimanjaro akemea kiburi kazini

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu akizungumza na Wafanyakazi wa Mkoa huo, katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushrika Moshi.Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewataka watumishi mkoani humo, kuacha kufanya kazi kwa  kiburi na kwa mazoea na badala yake wawahudumie wananchi kwa kufuata misingi na taratibu kwa kuwa ndilo jukumu lao muhimu lililowaweka ofisini.

Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewataka watumishi mkoani humo, kuacha kufanya kazi kwa  kiburi na kwa mazoea na badala yake wawahudumie wananchi kwa kufuata misingi na taratibu kwa kuwa ndilo jukumu lao muhimu lililowaweka ofisini.

Babu amesema wamepokea malalamiko mengi kuhusu baadhi ya watumishi na wanaendelea kuyafanyia kazi taratibu  kwa kuwa siyo kila jambo linalokuja, unamsimamisha, kukamata au kufukuza mfanyakazi, hivyo wataendelea kuelimishana taratibu ili wote waweze kuzungumza lugha moja.

Babu ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, mei 1,2023, wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ambapo katika Mkoa huo yamefanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi

"NItoe rai kwa wafanyakazi kufanya kazi kwa weledi zaidi, na kuzingatia taaluma zenu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea, pamoja na kuwa kiburi cha utumishi katika kutoa huduma kwa wananchi tunaowahudumia kwenye maeneo yote ya Mkoa wa Kilimanjaro, ama tunapotoa huduma kwa wafanyakazi wenzetu"

"Nawaomba sana wafanyakazi tuendelee kutoa huduma bora pamoja na changamoto tulizo nazo, usitoke nyumbani baba au mama amekuudhi unaenda kutoa hasira kwa mtu unayempa huduma, kwani tunapata malalamiko mengi lakini tunaendelea kuyafanyia kazi taratibu, siyo kila jambo linalokuja, unamsimamisha, kufukuza au kamata mfanyakazi, hapana tutaendelea kuelimishana taratibu ili angalau wote tuweze kuzungumza lugha moja"

Aidha mkuu huyo pia aliwataka wafanyakazi kuendeleza ushirikiano na mshikamano katika sehemu za kazi  baina ya wafanyakazi na wafanyakazi pamoja na wafanyakazi na waajiri katika kutekeleza majukumu yao.

Naye, Mratibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) mkoani hapa, Kanuti Magati amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili wafanyakazi mkoani humo, ni ushirikiano duni katika ofisi ya ofisa kazi Mkoa huo pamoja baadhi ya waajiri kutoa mikataba ya muda mfupi katika kazi ambazo ni endelevu.

"Sisi wafanyakazi tumekuwa tukikumbana na changamoto nyingi na tumekuwa tukikosa ushirikiano mzuri kutoka ofisi ya Afisa kazi pindi tunapopeleka malalamiko yetu,ushirikiano katika ofisi ile ni duni, na imekuwa ikipelekewa malalamiko kutoka kwa wafanyakazi," amesema.