RC Kunenge apata hofu chanjo Uviko-19 kuisha muda wake

Mkuu wa mkoa wa Pwani ,  Abubakar Kunenge

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuna chanjo 15,000 za Uviko-19 hazijatumika mkoani humo huku kukiwa na changamoto kwa kuwa baada ya mwezi mmoja kuanzia leo Jumamosi Septemba 25, 2021  zitafikia mwisho wa matumizi yake.

Pwani. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuna chanjo 15,000 za Uviko-19 hazijatumika mkoani humo huku kukiwa na changamoto kwa kuwa baada ya mwezi mmoja kuanzia leo Jumamosi Septemba 25, 2021  zitafikia mwisho wa matumizi yake.

Ameeleza kuwa mkoa umepata dozi  15,000  za chanjo ya Uviko-19 ambazo bado hazijatumika kati ya 30,000 zilizopokelewa, zitumike  katika kipindi kifupi kijacho.

Kunenge amesema  kwa kuanza wameamua kukutana na kamati ya afya ya msingi ngazi ya mkoa na wilaya, wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Tamisemi ili kwa pamoja kufanya tathimini na kujipanga upya kwa kuongeza wigo mpana wa utoaji chanjo hiyo ili iishe yote kabla ya muda wake wa kuharibika haujafika.

"Chanjo hizi zina muda wake maalumu na tumeangalia mpaka sasa katika mkoa wetu katika chanjo 30,000 tulizopokea sasa hivi tumefikia asilimia 50 ya dozi hizi kwa maana zimetumia kama 15,000 tu , nusu ya chanjo hizo bado hazijatumika na ni mwezi mmoja tu umebaki lazima tutumie mbinu shiriki na hizi zitumike kwa hiyo kikao hiki ni kikao cha kutafuta majibu," amesema Kunenge akibainisha kuwa idadi ya waliochanja ni ndogo ikilinganishwa na wakazi wa mkoa huo huku akitaka wakuu wa wilaya kusimamia utoaji wa chanjo.

Mganga mkuu wa Mkoa huo Dk Gunini Kamba amesema wamewaandaa watoa huduma 550 kupatiwa mafunzo kwa ajli ya kusambazwa kwenye vituo zaidi ya  200 zitakavyotangazwa kwenye mkoa huo idadi ambayo imeongezeka kutoka vituo 75  vya sasa .

Kamba ameweka wazi kuwa tangu Julai 30,2021  Mkoa huo ulipoanza kutoa  chanjo hakujatokea mtu yeyote aliyepata madhara ya kiafya bali zilizotokea ni changamoto ndogo ndogo za kawaida mfano kichwa kuuma na uchofu kero ambayo ni ya kawaida kwa chanzo zozote zinazotolewa kwa mara ya kwanza.

Baadhi ya washiriki wa kikao hicho  wakiwemo viongozi wa dini akiwemo Sheikh Khamis Mtupa na Mtawa Daria Mbumi  wamesema wataendelea kuelimisna jamii kuona umuhimu wa kuchanja.