Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RC Malima aagiza Halmashauri Morogoro kuwasaidia vijana kusajili bidhaa

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima (mwenye kofia) akitazama bidhaa za vijana wajasiliamali ambao ni wanufaika wa mradi wa Skills Employment awamu ya pili unaofadhiwa na Swisi Contact. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ina zaidi ya Sh300  milioni kwa ajili ya kusaidia vijana kupitia mikopo, ikiwemo ya asilimia 10 inayotolewa na kila halmashauri.

Morogoro. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, ameziagiza halmashauri zote za mkoa huo kuweka utaratibu utakaowasaidia vijana wajasiriamali kusajili bidhaa zao ili ziweze kutambulika kisheria na kupata fursa za masoko ndani na nje ya nchi.

Malima ametoa agizo hilo leo Juni 9, 2026 wakati akifungua Jukwaa la Ujuzi kwa Ajira lililofanyika mkoani Morogoro, ambalo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Skills for Employment Tanzania (SET) unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC) kupitia Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania.

Amesema Serikali ya mkoa ipo tayari kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuweka mikakati itakayowafikia vijana kwa urahisi, hasa katika kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na hata kuajiri wenzao.

“Changamoto inayowakabili vijana sio tu ukosefu wa mitaji, bali pia ni uamuzi wa kuchukua hatua. Nawaambia vijana wa Morogoro, yeyote mwenye changamoto yake akikwama aje ofisini kwangu. Nina zaidi ya Sh300  milioni kwa ajili ya kusaidia vijana kupitia mikopo, ikiwemo ile ya asilimia 10 inayotolewa na kila halmashauri,” amesema Malima.

Hata hivyo, amewataka vijana kuwa waaminifu wanapopewa mikopo hiyo, akisisitiza kuwa uzoefu unaonesha baadhi ya makundi ya vijana kuchelewa au kushindwa kurejesha kwa wakati tofauti na makundi mengine.

Kwa upande wake, Meneja wa Mafunzo wa mradi wa SET, Victoria Nkuba, amesema mradi huo unalenga vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24, kwa lengo la kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi na usindikaji.

Amesema mradi huo pia unakabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana kupitia mafunzo ya vitendo na uunganishaji na fursa za kiuchumi.

“Mradi umesaidia kuzalisha mazao ya mbogamboga, mahindi, ufugaji nyuki, kuku pamoja na usindikaji. SET ni mradi wa miaka 12 unaotekelezwa kwa awamu tatu, na sasa tupo awamu ya mwisho ambayo inatekelezwa Morogoro na Iringa,” amesema Nkuba.

Baadhi ya vijana walioshiriki jukwaa la ujuzi kwa ajili ya ajira lililofanyika mkoani Morogoro kama sehemu ya mradi wa Skills for Employment Tanzania (SET) unaofadhiliwa na Shirika la maendeleo na ushirikiano la Uswisi (SDC) kupitia ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania. Picha Hamida Shariff

Kwa mujibu wa Nkuba, mradi huo umefikia vijana 10,900 ambapo 4,199 kati yao ni wasichana, wakiwemo waliopata ujauzito wakiwa na umri mdogo kati ya miaka 15 hadi 24, na hivyo kushindwa kuendelea na masomo.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mkazi wa Swisscontact, Sebine Renggli, amesema lengo la kufikia vijana 10,900 limefanikiwa kwa asilimia 100, na sasa mradi umeingia awamu ya tatu inayolenga kuwawezesha zaidi wajasiriamali walioibuka katika awamu zilizopita.

Kwa upande wake, Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Nicole Providoli, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Uswisi na Tanzania katika kukuza ujuzi wa amali, akibainisha vipaumbele vitatu ambavyo ni kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, kuunganisha ujuzi na kipato, pamoja na kuhakikisha ujumuishi katika kila hatua ya maendeleo.

Miongoni mwa vijana walionufaika, Latifa Athmani, ambaye ni mlemavu wa ngozi, amesema mradi huo umemsaidia kuimarika kiuchumi kwa kuanzia bidhaa moja hadi kufikia zaidi ya bidhaa tatu.

Hata hivyo, amesema changamoto kubwa anayokutana nayo kwa sasa ni kukosa nembo ya kuthibitisha ubora wa bidhaa zake (barcode), hali inayompa ugumu kupanua soko na kuaminisha ubora wa bidhaa zake.