RC Mrindoko awapa siku saba waliofuja fedha za wakulima

Muktasari:

  • Mkuu wa mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko ametoa siku saba kwa viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) waliofuja fedha za wakulima na kuwasababishia umasikini wazirejeshe.


Katavi. Mkuu wa mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko ametoa siku saba kwa viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) waliofuja fedha za wakulima na kuwasababishia umasikini wazirejeshe.

Mrindoko ametoa agizo hilo leo Oktoba 13 wakati akizungumza na wadau wa kilimo kwenye kikao cha kufanya tathimini ya uzalishaji mazao msimu uliopita na kuweka mpango mkakati musimu wa kilimo ujao.

Amesema kuna malalamiko mengi wanayoyapokea kutoka kwa wakulima kuanzia kwenye uzalishaji wakati wa utolewaji mbegu na pembejeo zingine za kilimo zinazosimamiwa na Amcos.

“Shida zaidi ipo wakati wa masoko, ambapo viongozi wengi Amcos wamekuwa siyo waaminifu na wanatumia madaraka yao kuwadhulumu wakulima.

“Mkulima analeta zao lake lipimwe anaambiwa ni kilo 200 kumbe ni 300 zinazobaki zinakusanywa. Halafu naadaye zinauzwa kwakutumia majina hewa fedha zinaingia kwa viongozi. Nawatahadharisha msifanye mchezo tena na nafasi zenu na atayebainika hataachwa salama,” alisema Mrindoko.

Kwa upande mwingine, RC Mrindoko aliema mkoa huo umepanga kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kutoka tani 990,629 hadi kufikia tani 1.6 milioni kwa msimu ujao.

Kikao hicho cha kuzindua msimu wa kilimo 2021/2022 kimekwenda sambamba na wadau wa kilimo kuonyesha bidhaa na dhana mbalimbali zinazowawezesha wakulima katika shughuli zao.