RC Mtwara atoa saa tano taarifa urejeshwaji fedha za wakulima

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti. Florence Sanawa

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti ametoa saa tano ili kupata taarifa ya fedha za pembejeo ambazo bado hazijarejeshwa kwa wakulima kutoka vyama vikuu vya MAMCU na TANECU.

Mtwara. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti ametoa saa tano ili kupata taarifa ya fedha za pembejeo ambazo bado hazijarejeshwa kwa wakulima kutoka vyama vikuu vya MAMCU na TANECU.

Agizo hilo amelitoa leo Jumanne Mei 17, 2022 wakati wa uzinduzi wa pembejeo ambapo amesema kuwa hadi sasa ana taarifa ya Chama Kikuu cha Tandahimba & Newala Cooperative Union (TANECU) pekee kurejesha Sh2.2 bilioni kwa wakulima wake.

Amesema kuwa pamoja na taarifa hiyo pia anafahamu kuwa chama cha MAMCU bado hakijarejesha fedha ambapo vyama 8 kati ya 78 wameshawasilisha majina ya wanachama wao hivyo kuwataka vyama vilivyowasilisha majini warejeshewe fedha zao.

“Nataka nipate taarifa za fedha hizo wakulima wasihujumiwe Serikali imeshatoa maelekezo warejeshewe fedha hizo hatutakubali kuona mkulima anahujumiwa katika fedha hizi za pembejeo”

“Kama wapo wakulima ambao hawajapata pesa nimetoa namba yangu ya simu wanijulishe moja kwa moja nitasimamia hilo hakuna mkulima atakaehujumiwa katika zoezi hili namuagiza mrajisi ashirikiane nao ili kuhakiksiha kuwa kila mkulima amepata pesa zake”

“Lazima maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali yatekelezwe ni muhimu mfahamu kuwa unapokuwa kiongozi kuwa mwadilifu ama kuwa na nidhamu sio hiari ni lazima yote yanayopangwa lazima yalekelezwe” amesema Gaguti