RC Mwanza aagiza akaunti za maendeleo Buchosa zichunguzwe

Thursday June 23 2022
By Daniel Makaka.

Buchosa. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabliery ameagiza taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza akaunti za fedha za maendeleo Halmashauri ya Buchosa kutokana na upotevu wa Sh15 milioni.

Kauli hiyo ameitoa kwenye kikao maalumu cha baraza la madiwani la Halmashauri ya Buchosa cha kujadili hoja za mkaguzi mkuu wa Serikali (CAG).

Hali hiyo imekuja baada ya Sh15 milioni kuonekana zilihamishwa kutoka akaunti ya mapato ya ndani kwenda akuanti ya maendeleo, lakini hazijaonesha kupokelewa kwenye akaunti husika.

Amesema katika hoja ya ukaguzi inaonyesha taarifa ya benki na nyaraka za kuhamisha fedha inaonyesha kiasi cha Sh15 milioni kwenda kwenye akaunti ya maendeleo ya Juni 30, 2021 hazikuonekana kupokelewa kwenye akaunti hiyo.

Sambamba na matumizi yasiyo sahihi ya fedha zilizowekwa na wakusanyaji mapato wapatao 28 kwenye akaunti ya amana kama dhamana ya kazi, Sh18.5 milioni zinaonekana zilishatumika kwa shughuli nyingine kinyume na utaratubu.

"Halmashauri ya Buchosa imeonekana kama shamba la bibi licha ya kupata hati safi, hivyo uchunguzi unatakiwa kufanya ili kubaini watu waliohusika na hujuma hii wachukuliwe hatua," amesema Gabriel.

Advertisement

Halmashauri ya Buchosa ni miongoni mwa Halmashauri nane zinazounda Mkoa wa Mwanza, ambapo tangu ianzishwe mwaka 2015 imekuwa na mwenendo wa kupata hati safi licha la kupata hati ya mashaka kwa miaka miwili ya2016/17 na 2018/19.

Akizungumzia ubadhirifu huo, Diwani wa Kata ya Bulyaheke, Bageti Ngele amesema watumishi wamekuwa siyo waadilifu katika suala zima la usimamizi wa fedha, hivyo uchuguzi ukifanyika watakao bainika watachukuliwa hatua.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga ameahidi kufuatia suala hilo ili ukweli ubainike juu ya upotevu wa fedha hizo.


Advertisement