RC Njombe awataka wananchi ‘kutopagawa’ fidia Liganga, Mchuchuma

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka akihutubia wananchi wanaotarajia kupata fidia za Liganga, Mchuchuma

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Njombe Antony Mtaka awaasa wanufaika wa fidia za Liganga na Mchuchuma kutuliza akili na kupanga matumizi bora ya fedha zao za malipo ya fidia.

Ludewa. Mkuu wa Mkoa wa Njombe Antony Mtaka awaasa wanufaika wa fidia za Liganga na Mchuchuma Wilayani Ludewa kutowehuka na malipo hayo.

Ameyasema hayo leo Mei 18 2023 alipo fanya ziara wilayani Ludewa yenye lengo la kutoa elimu kwa wanufaika wa fidia za Liganga na Mchuchuma pamoja na wananchi wanao izunguka miradi hiyo.

Amesema matukio mengi ya ajabu yamekuwa yakijitokeza katika maeneo tofauti pindi fidia au fedha nyingi zinapo ingizwa kwa pamoja.

“Tumeshuhudia matukio mengi yanayojitokeza baada ya fedha kulipwa, tuliona Mtwara watu baada ya kulipwa fedha za korosho wakawa wanakunywa bia baada ya kuchoka wakanywesha mpaka mbuzi,” amesema Mtaka.

Ameongeza kuwa wao kama uongozi wa Mkoa wanatoa elimu ya matumizi bora ya pesa na uwekezaji ili wananchi hao wasije jutia mbeleni.

“Tunatoa elimu hivi ili majuto anavyokuja awe mjukuu wa kwelikweli, hatutaki pesa hii ivunje ukoo, isiwa farakanishe bali tafuteni vitu vya kufanya muwekeze, kuna watu watakuja kusimulia kuwa fulani alipata fidia lakini hali mbaya,” ameshauri Mtaka.

Kwa upande wake Katibu tawala Mkoa wa Njombe Judica Omary amewataka wananchi hao kuboresha makazi yao baada ya malipo.

“Muende mkaboreshe makazi yenu mapya katika eneo jipya mtakalo hamia kwasababu majengo yenu yana fidiwa, mtakavyo hama mkajenge nyumba bora Zaidi,” amesema Omary.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe Deo Sanga (Jah People) amewaomba Wana-Ludewa kumuombea Rais na wasaidizi wake.

 “Kwa kauli moja tuhakikishe tunamuombea Rais wetu kwa jinsi anavyo wajali wanaludewa, mmepewa miradi ya Maendeleo na sasa mnalipwa fidia ambayo ilikwama kwa mda mrefu,” amesema Mwenyekiti huyo wa CCM.

Na kwa upande wa Mbunge wa Ludewa Joseph Kamonga, anadhani Wananchi wanaopisha maeneo hayo baada ya kulipwa fidia wanayo haki ya kunufaika na miradi hiyo, kwa kupitia uwekezaji.